Historia ya mafanikio imeandikwa katika Bandari ya Tanga ambapo meli kubwa sita zenye urefu wa mita 150 hadi mita 200 zimeweza kuhudumiwa katika bandari hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu hali iliyopelekea shehena ya mizigo kuongezeka katika bandari hiyo.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Mei 25 , 2023 na Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha akiongea na waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo na kubainisha kuwa, mafanikio hayo yametokana na miradi mikubwa ya uboreshaji wa bandari hiyo iliyofanywa na serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Mrisha ameongeza kuwa, mradi wa uboreshaji wa bandari hiyo ulikuwa ni awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilihusisha kazi za kuongeza kina cha maji katika mlango bahari (entrance channel) na kuongeza upana mlango huo hadi kufikia mita 73.
Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 172. 3
Akizungumzia kuhusu mradi wa awamu ya pili ya uboreshaji wa bandari hiyo Mrisha amesema
“Awamu ya pili ilikuwa ni mradi wa kuboresha gati zote mbili kwa kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi 13 mradi, mradi ulianza Septemba 05, 2020 na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 256.8 ambapo hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 99.85 na unatarajiwa kukamilika Juni Mosi, 2023”
Mrisha ameendelea kwa kusema kuwa, mafanikio ambayo yemeshuhudiwa katika bandari ya Tanga kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali kupitia TPA ni pamoja na kuifanya bandari kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa, mapato kuongezeka, kuchochea ukuaji wa uchumi katika mikoa ya Kaskazini ikiwemo Tanga, Kilimanjaro, Arusha, kupunguza muda wa kuhudumia meli moja kutoka siku 8 hadi siku 4.
Faida nyingine ni pamoja mapato kuongezeka kufuatia ongezeko kubwa la shehena ya mizigo, ghafama za uendeshaji kupungua kufuatia kuwa na mpakuo mmoja wa mizigo kutoka mipakuo miwili (double handling) iliyokuwepo hapo awali, shehena ya mizigo kuongezeka kutoka tani 750,000 hadi kufikia tani milioni 3 kwa mwaka.
Kwa upande wake, mmoja wa wadau wa Bandari ya Tanga, Thorea Khalfan ambaye ni afisa mauzo kutoka kampuni ya kutoa huduma ya kutoa mizigo bandarini ya Topmax (T) Limited amesema, baada ya maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari ya Tanga ufanisi umeongezeka ambapo gharama za mipakuo (double handling) zimeondoshwa huku ikiwa hakuna msongamano wowote.
Thorea ameipongeza serikali ya awamu sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo na kuongeza kuwa hatua hiyo itatachochea ukuaji mkubwa wa uchumi katika Taifa.
Bandari ya Tanga ni moja ya bandari kongwe nchini ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 1988 na kukamilika mwaka 1991 ikiwa na ukubwa wa hekta 17 ikiwa na bandari ndogo ndogo nne ambazo ni Sahare, Pangani, Kipumbwi na Mkwaja ambapo miongoni mwa bidhaa zinazosafirishwa na bandari hii ni pamoja na Katani, Kahawa, mbao na macadamia (karanga pori)