Mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili, Sinach, anakabiliwa na kesi ya shilingi bilioni 25 katika Mahakama Kuu ya Lagos, iliyofunguliwa na mtayarishaji wa muziki Michael Oluwole, anayejulikana kama Maye.
Oluwole anadai alichangia mafanikio ya wimbo maarufu Way Maker kwa kurekodi, kuchanganya, na kufanya mastering, pamoja na kuunda vyombo kama piano na synthesizers.
Hata hivyo, anadai hajalipwa stahiki zake, na wimbo huo umetengeneza mapato makubwa tangu kutolewa kwake mwaka 2015.
Sinach, kwa upande wake, anasisitiza kuwa yeye ndiye mtunzi na muimbaji wa wimbo huo, huku wakili wake, Emeka Etiaba, akisema Maye alilipwa $300 kwa huduma za mixing na kufanya mastering pekee.
Kesi hii imeibua mjadala kuhusu haki za mali–miliki, fidia kwa wachangiaji wa kazi za sanaa, na umuhimu wa makubaliano rasmi kwenye sekta ya muziki.
Kabla ya msanii wa nyimbo za injili wa Nigeria Sinach (Osinachi Kalu Okoro Egbu) na mtayarishaji Michael Oluwole kutayarisha wimbo maarufu wa kimataifa wa “Way Maker,” walikuwa washirika ambao walifanya kazi katika nyimbo mbalimbali za injili wakati wa Sinach kama muumini wa kanisa kubwa la Nigeria, Christ Embassy.
“Way Maker” ulikuwa wimbo wa kwanza na pekee waliotoa, na kumpa Sinach mafanikio yake makubwa kibiashara ambapo wimbo huo pia ni kiini cha kesi inayotarajiwa kuanza kusikilizwa Novemba 27 inayowahusisha Oluwole na Sinach.