Rais mpya wa Msumbiji Daniel Chapo, wa chama tawala cha FRELIMO, ameapishwa rasmi kuwa rais wa Msumbiji katika hafla ya faragha iliyofanywa chini ya ulinzi mkali mjini Maputo.
Kuapishwa kwake kunafuatia miezi kadhaa ya machafuko yaliyosababisa vifo vya watu 300, kulingana na kundi la waangalizi wa uchaguzi la Plataforma Decide.
Katika hotuba yake, Bw. Chapo ameahidi kuzingatia umoja na kuongoza juhudi za maendeleo kote nchini.
Biashara nyingi mjini Maputo zilifungwa baada ya mgombea urais aliyeshindwa Venâncio Mondlane kuitisha mgomo wa kitaifa kupinga kuapishwa kwa Chapo.
Chapo alishinda uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana kwa asilimia 65 ya kura, na kuendeleza utawala wa miaka 49 wa chama cha Frelimo.
Mondlane – ambaye aliwania urais katika uchaguzi huo kama mgombea huru – alishika nafasi ya pili kwa 24% ya kura. Alipinga matokeo hayo akisema yamechakachuliwa.