MTANDAO wa Elimu Tanzania (TENMET) umesema umefanikiwa kuchochea maendeleo ya elimu nchini, tangu ilipoanza kuratibu mradi wa ufuatiliaji na kufanya tathmini ya kazi zinazofanyika kwenye jamii kupitia fedha zilizotolewa katika utekelezaji wa masuala ya elimu.
Program hiyo inayosimamiwa na TENMET ilianza utekelezaji wa majukumu yake Septemba 2022 na inatarajiwa kukamilisha Machi mwaka huu, na jana ilikutana na taasisi 10 wanazoshirikiana katika utekelezaji wa mradi huo unaofanyika katika mikoa 10 ambayo ni Dodoma, Rukwa, Katavi, Pwani, Njombe, Iringa, Morogoro, Mtwara, Tanga na Lindi.
Akizungumza na waandishi wa habari Msimamizi wa Program hiyo kutoka TENMET Matha Makala, alisema matokeo waliyoyapata ndani ya miezi sita ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo ni kuanzishwa kwa kamati za ufuatiliaji na tathimini ya rasilimali za umma kwenye sekta ya elimu katika maeneo ambayo hayakuwa nazo.
Pia alisema ndani ya miezi sita tangu kuanza kwa utekelezaji wamefanikiwa kuchochea ujenzi wa miundombinu ambayo haikuwa imekamilika ikiwemo vyoo na madarasa, na kwamba kamati ziliamsha hari na kuonyesha umuhimu wa wananchi kwenye kufuatilia rasilimali za umma.
Samson Mnyawami kutoka taasisi ya MMADEA, inayotekeleza mradi huo katika wilaya ya Kilolo, mkoani Morogoro, alisema katika utekelezaji wa program hiyo walibaini kuwepo kwa upungufu wa vifaa vya kufundishia ikiwemo vitabu katika shule wilayani humo na kutokuwa na uwiano wa walimu na wanafunzi, kwa darasa moja kuwa na zaidi ya wanafunzi 80.
“Kwa mfano katika kijiji cha Tailum kata ya Ilum wanafunzi kutembea na wanakijiji ni jambo la kawaida na wananchi wanakiri na walimu kutembea na wanafunzi lakini hawawezi kuwachukulia hatua yoyote na akimaliza darasa la saba anaolewa, hii inachangia kuthoofisha elimu,” alisema Samson.