Mahakama ya Guinea siku ya Jumatano ilimhukumu kiongozi wa zamani wa kijeshi Moussa “Dadis” Camara kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumpata na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mauaji ya uwanja wa michezo ya mwaka 2009 yaliyofanywa na jeshi na kuua takriban watu 157 na kuwaacha makumi ya wanawake kubakwa.
Mahakama ya Jinai ya Guinea ilimtia hatiani Camara na maafisa wengine saba wa vyeo vya juu baada ya kesi ya muda mrefu juu ya mashtaka ya mauaji, utekaji nyara na ubakaji ambayo yalitajwa tena kama “uhalifu dhidi ya ubinadamu” siku ya Jumatano.
Washtakiwa wengine wanne waliachiliwa huru.
Zaidi ya manusura 100 na jamaa za wahasiriwa walitoa ushahidi katika kesi hiyo iliyoanza Novemba 2022, zaidi ya muongo mmoja baada ya mauaji hayo na chini ya shinikizo kutoka kwa familia na wanaharakati wanaodai haki itendeke.
Waandamanaji kwenye uwanja wa michezo Septemba 2009 walikuwa wakipinga mipango ya Camara kugombea urais wakati wanajeshi walipowafyatulia risasi na kuwabaka makumi ya wanawake. Kiongozi wa wakati huo wa kijeshi alikuwa amefanya mapinduzi mwaka uliopita.
Wanajeshi wakati huo walisema “vitu visivyodhibitiwa” vya jeshi vilitekeleza ubakaji na mauaji. Lakini wasaidizi wakuu wa Camara walikuwa uwanjani na hawakufanya lolote kukomesha mauaji hayo, ripoti ya Human Rights Watch ilisema.