Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amemuagiza Mthamini Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Ardhi kufika Mbeya ndani ya siku mbili ili kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika eneo la Uyole na wakazi wa mtaa wa Sae na Ituha jijini Mbeya.
Waziri Silaa amefikia maamuzi hayo baada ya kufanya ziara katika eneo lenye mgogoro wa Taasisi hiyo na wakazi wa mtaa huo ambao wanadaiwa kuwa ni wavamizi wa eneo hilo ili kuanza mchakato wa uthamini na ulipaji fidia.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Geophrey Mkamia ameeleza namna TARI ilivyo jitahidi kushirikisha wakazi hao katika kutatua tatizo hilo bila mafanikio. Aidha ameeleza pia umuhimu wa eneo hilo lenye faida kwa Taifa.
Baada ya kusikiliza kwa makini maelezo hayo Waziri Silaa aliamua kumpigia simu Mtamini Mkuu wa Serikali Eveline Mgasha na kumtaka kufika jijini Mbeya ndani ya Siku mbili akiambatana na Kamishna wa Ardhi Mathew Nhonge ili kuharakisha utoaji maamuzi ya mgogoro huo.