Michezo

Mchezaji mkongwe wa Mtibwa anusurika kukatwa mapanga na mashabiki

on

Kikosi cha MtibwaKIUNGO mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kisiga ‘Marlone’, amenusurika kukatwa mapanga na mashabiki wa timu ya Faru Jeuri wakati akiichezea Daladala FC katika mechi ya Kombe la Ng’ombe kwenye Uwanja wa Snai uliopo Vingunguti, Dar es Salaam.

Mbali ya Kisiga wachezaji wengine wa Ligi Kuu Bara na waliowahi kucheza ligi hiyo ambao waliichezea Daladala ni Buji Selemani aliyewahi kucheza JKT Ruvu na beki wa Kagera Sugar, Salum Kanoni huku Faru Jeuri ikiundwa na beki wa Ashanti United, Tumba Sued na Salum Machaku wa JKT Ruvu.

Tukio lilianza kama sinema, haikueleweka sababu kwani wakati timu zikijiandaa kuingia uwanjani kuanza mchezo, mashabiki wa Faru Jeuri wakiwa na mapanga na visu walimvamia Kisiga kwa nia ya kumkata baadhi ya sehemu za mwili wake.

Baada ya kuona hali hiyo, mashabiki wa Daladala nao walivamia uwanja kumwokoa Kisiga na kumwondoa eneo la tukio.

Kutokana na tukio hilo wachezaji wa Daladala na mashabiki waligoma kuendelea na mchezo huo kwa kuhofia usalama wao.

Waandaaji wa michuano hiyo nao walikubali kuahirisha mechi kutokana na hofu hiyo ya usalama.

Hata hivyo ili kuzuia uwezekano wa jambo hilo kutokea tena, waandaaji hao wameimarisha hali ya usalama katika mechi za mashindano hayo.

Mwanaspoti lilipowasiliana na Kisiga kuhusu tukio hilo alisema: “Achana na habari za mechi hizo za mitaani.

Sitaki kuzizungumzia, sasa nipo kambini na timu yangu ya Mtibwa Sugar.”

Tupia Comments