Watu watano wamefariki Dunia mkoani Kagera, kufuatia matukio mawili tofauti yaliyotokea, katika wilaya ya Ngara na Muleba, akiwamo mtoto mmoja mwenye umri wa miaka kumi aliyekufa maji, wakati akivua Samaki katika Ziwa Victoria.
Akizungumza leo Disemba 20, 2019, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Revocatus Malimi, amesema kuwa tukio la kwanza limetokea katika Kijiji cha Kihinga, wilayani Ngara, ambapo watu watatu Sinzumusi Gerald, Minani Ramadhan na Muhambazi Severine wote Raia wa Burundi, waliokuwa wakifanya shughuli za kuchimba madini aina ya ORPHRAM na TANTALITE, walifariki ndani ya shimo baada ya kukosa hewa.
Aidha katika tukio la pili Kamanda huyo amesema kuwa watu wawili waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria, eneo la Ilemela wilayani Muleba, ambao ni Robson Juvenary, mwanafunzi wa darasa la tatu, Shule ya Msingi Kiga na Christian Paul, wamefariki Dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia kupigwa na wimbi na kupinduka.