Ni vilio na simanzi vikitawala eneo la Kamachumu lililopo Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera ulipokutwa mwili wa mtoto Asimwe Novart mwenye miaka miwili na nusu aliyekuwa albino huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimekatwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Polisi Mkoa Kagera iliyotolewa June 6 mwaka huu ilieleza kuwa mtoto huyo aliibwa nyumbani kwao May 30 mwaka huu 2024 na mwili wake umepatikana jana June 17,mpaka sasa watu wanne wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi akiwemo baba Mzazi wa mtoto huyo
Katibu Tawala Wilaya ya Muleba Benjamini Mwikasyege amefika eneo la tukio na kueleza kuwa mwili huo umekutwa umefungwa kwenye mfuko na kutelekezwa kwenye karavati iliyopo barabara ya Ruhanga-Makongora kata ya Ruhanga,Tarafa ya Kamachumu,Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera huku akisema wamekuta baadhi ya viungo vyake vikiwa vimekatwa.
Aidha Mwikasyege amelaani kitendo hicho huku akieleza kuwa mwili wa mtoto huyo umechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na utaratibu utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu lakini wao kama serikali watahakikisha wanasimamia utaratibu wote wa kupumzishwa mtoto huyo.