Mtoto wa miezi miwili ameuawa baada ya kuanguka ndani ya sufuria la uji wa moto baada ya mzozano wa Ksh.1700 (Tsh 27,922) zikiwa ni pesa za ‘Chamaa’ vikiwa ni vikundi kidogo vya kusaidiana vinavyojulikana huku Tanzania kama vikoba au upatu. Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Koduol ‘B’, iliyoko katika kaunti ya Homa Bay, nchini Kenya.
Mtoto huyo aliyetambulika kwa jina la Sheldon Churchill alianguka kwenye uji uliokuwa unachemka jikoni wakiwa nyumbani kwa mama yake pindi ambapo wanachama hao walipofika na kudai malipo ya pesa ambayo walikuwa wanamdai mama huyo.
Mama mzazi wa mtoto huyo Sharon Auma (19) anasema wanachama na ‘Chamaa’ wapatao 20 waliingia nyumbani kwake kudai pesa lakini yeye hakuwa na kiasi hicho cha fedha hivyo kusababisha mzozano mkubwa kati yao, akieleza kuwa alikuwa amekopa mkopo wa Ksh.2500 (Tsh 41,062) kutoka kwenye ‘Chamaa’ lakini alikuwa amelipa Ksh.800 (Tsh 13,140) pekee.Wanakikundi hao walimwambia Sharon alipe Ksh.1700 iliyobaki au malii zake zingepigwa mnada.
Kulingana citizen digital, ugomvi huo ulizidi kuwa mkubwa wakati wanachama wa kikundi hicho walipoamua kuchukua magunia 16 ya mahindi makavu ili kulipa deni hilo. Sharon Auma alidai kuwa wanawake wawili walimsukuma pale alipokuwa akijaribu kuwadhibiti ili wasiingie kwenye chumba alichohifadhia magunia ya mahindi, kupelekea mtoto aliyekuwa amembeba kuangukia sufuria la uji. Kwa mujibu wa Benson Adongo mtoto huyo wa kiume alifariki alipokimbizwa hospitali ya rufaa ya Homa Bay.