Muingizaji wa kimataifa John Dumelo Raia wa Ghana amefanikiwa kukamilisha kutengeneza filamu iliyopewa jina la “Mulasi the death” katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti na bonde la Ngorongoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha mara baada ya kukamilika kurekodi filamu hiyo, Dumelo alisema filamu hiyo itakamilika mwakani na kuanza kuonekana kuonekana nchi mbalimbali duniani.
Alisema amefurahi kutengeneza filamu Tanzania katika hifadhi za wanyamapori kwani ni maeneo ya yanayovutia na kumpa uzoefu mpya kuokana na mazingira ya asili lakini pia akivutiwa Zaidi na Bonde la Ngorongoro ambalo ni moja ya maajabu saba ya Dunia na hifadhi ya Serengeti ambayo ina wanyama wa kila aina.
“Naimani filamu hii ikitoka itasaidia sana kutangaza vivutio vya Utalii wa Tanzania duniani lakini pia itawavuta wasanii wengine duniani kuja Tanzania kutalii na kutengeneza filamu”
Amewaasa wasanii wa Tanzania na Afrika nzima kuanza kubadili mitizamo na kuanza kuigiza katika vivutio mbalimbali badala ya mahotelini,vijijini na kwenye miji mikubwa.
Dumelo pia aliahidi kurudi tena Tanzania kuja kutengeneza filamu katika visiwa vya Mafia, Mkurugenzi wa filamu hiyo, Mtanzania anayeishi Marekani, Honeymoon Aljabri alisema filamu hiyo ya “MULASI THE DEATH”ambayo ameiandika ina maana Rafiki yangu kwa lugha ya Kigogo,inaeleza jinsi wasichana wanne wanavyoweza kukabiliana na msongo wa mawazo kwa kufanya utalii katika mbuga za wanyama.
“Wasichana hao ambao ni marafiki wanatoka Dodoma wanachukua trip kwenda Serengeti kwa ajili ya kupunguza msongo wa mawazo kumliwaza mwenzao kufanya utalii wa ndani na kupatatiba ya msongo wa mawazo badala ya kukata tamaa ya maisha”
Honeymoon alisema anashukuru mchango wa shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA), Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kampuni ya utalii ya Mauly Tours kwa mchango mkubwa ambao wametoa kukamilisha filamu hiyo.
Mkurugenzi wa Mauly tours Mozzah Mauly alisema ujio wa msanii huyo nchini ni kazi nzuri ya kutangaza Tanzania na vivutio vyake ambayo inafanywa na Rais Samia Suluhu , wizara ya maliasili na Utalii na chama cha mawala wa Utalii(TATO).
“filamu hii itakwenda kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuendelea kuvutia watalii kuja nchini kwani sasa dunia inajua Tanzania ni salama kwa watalii kuja”
Mozzah amesema kupitia filam hii na mwigizaji huyu wantarajia watapata wasanii na watu wengi mashuhuri ambao watakuja kutembelea vivutio vya utalii nchini.