Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora limeazimia kufukuzwa kazi kwa aliyekuwa Muuguzi wa Zahanati ya Kalunde, Elipidius Kweyamba, baada ya kupatikana na hatia ya kubaka mwanafunzi na kumpa mimba.
Akitangaza maamuzi ya Kamati ya nidhamu katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika Alhamis, Machi 11, 2021, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Ramadhan Kapela, amesema wamefikia hatua hiyo baada ya mtumishi huyo kupatikana na hatia ya kubaka hivyo kuhukumiwa na mahakama miaka 30 jela.
Amesema hukumu hiyo ilitolewa Septemba mwaka jana baada ya mtumishi huyo kupatikana na hatia ya kumwingilia kimapenzi kwa nguvu mwanafunzi na kumpa ujazito.
“Baraza limeafiki kufukuzwa kazi Muuguzi huyo baada ya kujiridhisha kuwa alikiuka maadili ya utumishi wa umma na hata baada ya kusomewa hukumu hakukata rufaa kama sheria inavyoeleza, hivyo tumemfukuza kazi rasmi,” amesema.
Aidha, Mstahiki Meya ameongeza kuwa mtumishi mwingine, Rehema Mussa (Muuguzi katika Zahanati hiyo) amesamehewa na kurejeshwa kazini na atakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi 6 baada ya kupatikana na hatia ya kutofika kazini kwa siku 37.