Kliniki moja huko Hais, magharibi mwa Yemen, imejaa watu wanaodhaniwaa kuwa na kipindupindu baada ya mvua kubwa na mafuriko kuikumba nchi hiyo. Eneo hili, ambalo limeathiriwa na vita kwa muongo mmoja, linakabiliwa na wimbi la wagonjwa huku wahudumu wa afya wakipambana kwa nguvu kubwa.
Daktari Bakil al-Hadrami ameeleza kwamba wingi wa wagonjwa umeongezeka kutokana na mafuriko, na huduma zinaweza kuanguka ikiwa hali haitadhibitiwa.
Kufuatia mafuriko yaliyotokea tangu mwisho wa Julai, takriban watu 60 wamepoteza maisha na wengine 268,000 wameathirika. Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Yemen ina kesi karibu 164,000 zinazohisiwa kuwa kipindupindu, na idadi hiyo inatarajiwa kupanda hadi 250,000 ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa. Hali ya mvua na mafuriko inachangia kuenea kwa kipindupindu kutokana na uchafuzi wa maji.
Msaada wa kimataifa unahitaji kuimarishwa mara moja ili kukabiliana na janga hili. Mafuriko pia yamesababisha kuharibu miundombinu, hali inayoongeza hatari kwa wale wanaojaribu kufikia jamii zilizoathirika. Hais, ikiwemo maeneo mengine, inakabiliwa na changamoto kubwa za kibinadamu, na hali hii inahitaji hatua za haraka ili kupunguza madhara ya kipindupindu.
Yemen inakumbwa na changamoto za muda mrefu kutokana na vita, uhaba wa maji, na miundombinu ya afya iliyoharibika. Umasikini na lishe duni vimeongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa kama kipindu-pindu, na mafuriko ya hivi karibuni yamekuwa kikwazo kingine katika juhudi za kutoa msaada.