Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mvua kubwa na mafuriko vinatatiza usafirishaji wa misaada katika nchi za Sudan, Chad na Sudan Kusini.
Taarifa hii imetolewa wakati hali ya kibinadamu katika nchi ya Sudan iliyokumbwa na vita inazidi kuwa mbaya, huku zaidi ya nusu ya wakazi wa nchi hiyo wakisumbuliwa na njaa.
Msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Sudan, Leni Kinzli amesema: Ingawa malori ya misaada yamekwenda hadi Darfur, lakini usafiri unatatizwa na barabara zilizojaa maji na matope. Hivyo tunahitaji njia nyingine ili tuweze kuongeza msaada, kuokoa maisha na kuzuia kuenea njaa.”
Mvua hiyo imezidisha mgogoro na hali mbaya ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita vinavyoendelea nchini Sudan, ambavyo vilianza mwezi Aprili mwaka jana kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Ripoti zinasema, kati ya watu zaidi ya 317,000 walioathiriwa na mvua kubwa na mafuriko, 118,000 wamelazimika kuyahama makazi yao. Sudan pia inakabiliwa na mlipuko wa kipindupindu unaosababishwa na mafuriko na maji machafu