Jeshi la polisi Mkoani Mara linawashikilia watu 22 kwa kuhusika na matukio mbalimbali ikiwemo mauaji ya Mwalimu wa Shule ya Msingi Busambara katika halmashauri ya wilaya ya Musoma, Dickson James aliyeuawa na kuporwa pikipiki yenye Namba za usajili MC 179 CYQ aina ya Super Tiger.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Longinus Tibishubwamu tukio hilo limetokea katika Kitongoji cha Nyakato, Kijiji cha Nyang’oma ambapo mwili wa mwalimu huyo ulikutwa ukiwa umetelekezwa mashambani huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa kamba.
Kamanda Tibishubwamu amesema jeshi hilo la polisi limekamata vitu mbalimbali katika msako maalumu wa kufunga mwaka, iliyoanza 26 Oktoba 2021 hadi 09 Disemba 2021 katika halmashauri zote za Mkoa huo kwenye maeneo ya majini na nchi kavu.
Ametaja mali za wizi zilizokamatwa kuwa ni Pikipiki 12, Magodoro 11 likiwemo Moja la Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kwangwa, Redio Nane za aina tofauti na Jenereta Moja, Televisheni 14, Simu janja aina tofauti Sita, Kompyuta mpakato Tatu, Ndoo za Rangi Mbili, Mitungi ya Gesi Sita,Vichwa vya Cherehani Viwili na Mashine za kusukumia maji Mbili.
Pamoja na hayo, amesema wameabaini Stoo bubu iliyokuwa ikitumiwa kuhifadhi mali za wizi, katika Mtaa wa Nyakato Mlimani, Manispaa ya Musoma na ilipopekuliwa kulikutwa Viti vya Plastiki 46 na Keni Tano mali ya Kiwanda cha Maziwa cha Musoma Diary.