Mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Rohila iliyopo Mbalizi, mkoani Mbeya, Laurence Mwangake amelazwa Hospitali ya Ifisi iliyopo mjini humo, ikidaiwa kuwa walimu wanne na walinzi wawili walimfungia katika chumba kumuadhibu, hali iliyomsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Imedaiwa kuwa sababu ya kumuadhibu mwanafunzi huyo anatuhumiwa kudokoa maandazi manne yaliyokuwa ndani ya duka la shule Februari 12 mwaka huu 2023.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ifisi, Dk. Hamis Bakari Ally amesema wamempokea mwanafunzi huyo akiwa na majeraha kichwani, mkononi, goti na miguuni lakini anaendelea vizuri.
Dk. Ally amesema mwanafunzi huyo alieleza kupata majeraha baada ya kudokoa maandazi akidai alikuwa na njaa.
Hata hivyo Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Ernest Hinju amesema maelezo ya awali ya mwanafunzi huyo ni kunyimwa chakula, ndipo akaenda kudokoa maandazi manne katika duka la shule, lakini mwalimu aliyefahamika kwa jina la Petro anadai hakumshambulia bali Mwanafunzi aliruka dirishani akikimbia adhabu ndipo akapata majeraha, hivyo uchunguzi unaendelea kuthibisha mazingira ya tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishana Msaidizi wa Polisi ACP, Benjamin Kuzaga amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba walimu na walinzi waliohusika na tukio hilo wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi na kwamba baada ya uchunguzi kukamilika atatoa taarifa kamili.