Mwanajeshi wa Urusi anayekabiliwa na kesi ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine, Vadim Shishimarin (21) amekiri kosa la kumuua raia ambaye hakuwa na silaha, Mwanajeshi huyo anatuhumiwa kwa kumpiga risasi Mzee wa miaka 62 siku chache baada ya vita nchini Ukraine kuanza.
Waendesha mashtaka wanasema kesi zaidi zinakuja, baada ya kubaini kuna uwezekano wa uhalifu mwingine wa kivita umefanywa na Wanajeshi wa Urusi, hata hivyo Urusi imekanusha kuwa Wanajeshi wake wamewalenga raia.
Kesi hiyo ni ya kwanza ya aina yake tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulipoanza mwezi Februari na imefanyika Kyiv, Ukraine, huku mkalimani akitafsiri kesi katika lugha ya Kirusi kwa Mshtakiwa ambaye ameulizwa kama anakubali hatia yake na akajibu ndio.
Anatuhumiwa kumuua raia huyo, ambaye inadaiwa alikuwa kwenye baiskeli katika eneo la mashariki la Sumy tarehe 28 Februari, siku nne baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Waendesha mashtaka wanasema Shishimarin alikuwa akiendesha gari lililoibwa akiwa na Wanajeshi wengine ndipo walikutana na mwendesha baiskeli huyo mwenye umri wa miaka 62 akitumia simu na kumpiga risasi ili kuzuia kuwaambia Watetezi wa Ukraine kuhusu eneo lao.