Brooke Bruk-Jackson mwenye umri wa miaka 21 alitawazwa kama miss Universe Zimbabwe, ambayo ina maana kwamba atawakilisha taifa la Afrika katika shindano lijalo la Miss Universe.
Shindano la urembo la Miss Universe Zimbabwe lililofanyika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22 wiki iliyopita, lilizua utata wa rangi katika nchi hiyo ya Afrika, huku wengi wakidai kuwa mshindi si mwakilishi sahihi wa wakazi wa Zimbabwe.
Mzaliwa wa Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, Brooke Bruk-Jackson pia ni mzungu, ambapo kwa wengi jambo hilo limekuwa ni tatizo na kutawazwa kwake kama Miss Universe Zimbabwe kulizua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii, huku wakosoaji kwasauti wakisema kuwa taji lake limechafuliwa na ubaguzi wa rangi, na kwamba alishinda kwa sababu tu ni mzungu.
Miss Universe Zimbabwe ni tukio la awali la kitaifa ambalo kupitia kwake mwakilishi wa nchi kwenye shindano la Miss Universe huchaguliwa.
Washiriki wanawakilisha majimbo 10 ya taifa la Zimbabwe na ni pamoja na raia wa Zimbabwe wanaoishi ughaibuni.