Kilichotarajiwa kuwa wakati wa furaha kwa ndoa ya Wanandoa hawa kutoka China kimegeuka kuwa chanzo cha kutoaminiana na wasiwasi baada ya kuzaliwa kwa mtoto wao, hali iliyosababisha Mume kudai kipimo cha DNA kutokana na rangi ya Mtoto kuwa tofauti na matarajio yake.
Gazeti la China Times limeripoti kisa hicho cha Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 30 kutoka Shanghai ambaye sasa anajitahidi kuokoa Ndoa yake kufuatia tukio hilo.
Kisa hichi ambacho kimevutia maoni mengi kwenye mitandao ya kijamii huko China kilianza kupata umaarufu baada ya Mwanamke huyo kueleza hadithi yake kwenye Mitandao ya kijamii, akiomba ushauri wa kina Mama wengine jinsi ya kukabiliana na hali hiyo, akisimulia tukio hilo alieleza mshangao wa Mume wake alipomwona Mtoto kwa mara ya kwanza, alipomkataa na hata kukosa kuonyesha shauku ya kumshika.
Hata hivyo, licha ya kukubali kipimo cha DNA ili kuthibitisha uaminifu wake, Mama huyo alikiri kuhisi huzuni kutokana na tabia ya Mume wake na Kulingana na ripoti, chapisho lake kwenye mtandao wa Weibo kutoka huko China lilipata jumbe nyingi za kumtia moyo zikieleza kuwa ni jambo la kawaida kwa Watoto wachanga kuwa na rangi ya ngozi tofauti pindi wanapo zaliwa.
Pia Wataalamu walijitokeza kumhakikishia kuwa ngozi ya Watoto wachanga inaweza kuwa na rangi hiyo kutokana na upungufu wa mzunguko wa Damu na ngozi nyembamba na kuwa rangi hiyo hupungua kadiri wanavyokua, baadhi ya Watu walimshauri pia azungumze na Mume wake kuhusu mustakabali wa uhusiano wao mara baada ya majibu ya kipimo kutolewa.