Mahakama mjini Bangkok ilimpata na hatia Sararat Rangsiwuthaporn, 36, raia wa Thailand na kumpatia hukumu ya kifo katika kesi ya kwanza kati ya msururu wa kesi anazotuhumiwa kuwaua marafiki zake 14 kwa kutumia sumu.
Matukio mengine ni pamoja na kuweka sumu kwenye chakula na kinywaji cha rafiki yake tajiri walipokuwa safarini mwaka jana.
Jamaa wa aliyeuwawa walikataa kukubali kwamba alikufa kifo cha kawaida na uchunguzi wa maiti ulipata athari za sumu kwenye mwili wake. Polisi walimkamata Sararat na kufichua vifo vingine kama hivyo kuanzia mwaka 2015. Mtu mmoja alinusurika.
Polisi wanasema Sararat, alikuwa na uraibu wa kucheza kamari na aliwalenga marafiki waliokuwa wakimdai pesa, kisha akawaibia vito na vitu vyao vya thamani.
Polisi wanasema, Sararat alisafiri na rafiki yake Siriporn Khanwong, 32, hadi mkoa wa Ratchaburi, magharibi mwa Bangkok mwezi Aprili 2023, ambapo walishiriki katika ibada ya Wabudha kwenye mto.
Wachunguzi wanasema, Siriporn alianguka na kufa baada ya kula na Sararat, ambaye hakufanya bidii ya kumsaidia.
Mabaki ya sumu yalipatikana kwenye mwili wa Siriporn, huku simu yake na pesa vikiwa havipo alipopatikana, walisema polisi.