Mwanamume mmoja kutoka Ufaransa mwenye umri wa miaka 71 anakabiliwa na mashtaka ya kuwahusisha zaidi ya wanaume 50 kumbaka mke wake mzee kwa zaidi ya miaka kumi bila yeye kufahamu.
Mwanamume huyo, ambaye alikuwa mfanyakazi wa zamani wa shirika la umeme la Ufaransa, EDF, alitumia dawa za kumlewesha mke wake ili asipate fahamu wakati wa unyanyasaji huo wa kijinsia.
Kulingana na wakili wa mke huyo, Antoine Camus, mwanamke huyo aliteseka kwa muda mrefu bila kujua, kwani alikuwa akiwekewa dawa za kumlewesha kila wakati alipobakwa. Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 68, aligundua unyama huo baada ya miaka mingi ya ndoa, na sasa ameazimia kukabiliana na mume wake pamoja na wanaume waliohusika katika kesi hiyo.
Unyanyasaji huo wa kijinsia ulianza mwaka 2011 wakati wenzi hao wakiishi karibu na Paris, na uliendelea hadi walipohamia Mazan, kusini mwa Ufaransa. Mwanamume huyo alitumia tovuti za mtandaoni kuajiri wanaume wengine wa kigeni ili kumbaka mke wake bila yeye kufahamu, kama ilivyofichuliwa na mazungumzo ya mtandaoni yaliyochunguzwa na polisi.
Polisi wa Ufaransa walianza kuchunguza kisa hicho mnamo Septemba 2020 baada ya kumkamata mwanamume huyo akirekodi kwa siri wanawake wengine watatu kwenye duka moja. Uchunguzi zaidi kwenye kompyuta yake uligundua maelfu ya picha na video za mke wake akiwa amepoteza fahamu, zikionyesha matukio mbalimbali ya ubakaji yaliyotokea nyumbani kwao.
Kwa jumla, wanaume 72 walihusishwa katika kesi hii, ambapo 51 walitiwa mbaroni na kushitakiwa. Kesi hiyo ya umma inatarajiwa kumalizika ifikapo Desemba mwaka huu.