Shutuma za “uchawi” ambazo zimekuwa zikitolewa tangu mwanzoni mwa Oktoba dhidi ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Ushelisheli, Patrick Herminie, zimeondolewa, ofisi ya mwendesha mashtaka wa Victoria imesema siku ya Alhamisi.
Wakati wa kufunguliwa mashtaka, Patrick Herminie, kiongozi wa chama cha United Shelisheli na mgombea katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2025, alishutumu uamuzi wa kisiasa.
“Ninaondoa mashtaka yote dhidi ya Patrick Herminie,” ofisi ya mwendesha-mashtaka wa Victoria imesema. Mashtaka yalifutwa kwa watu watano kati ya wanane walioshtakiwa, upande wa mashtaka umeongeza.
“Hakuna kesi dhidi yangu, kilichotokea ni hatua mbaya tu,” Patrick Herminie amewaambia waandishi wa habari baada ya kutoka mahakamani.
Patrick Herminie, pamoja na Washelisheli wengine sita na raia wa Tanzania, walikuwa wamefunguliwa mashtaka kama sehemu ya uchunguzi uliofunguliwa kwa “uchawi” na vile vile kwa “vitendo visivyo vya asili na ushirikina”. Kesi hiyo inahusishwa na kugunduliwa mwezi Agosti kwa miili ya mwanamke mzee na kijana mmoja iliyofukuliwa katika makaburi katika kisiwa kikuu cha Mahé.