Mahakama moja katika mkoa wa Wakayama uliopo magharibi mwa Japani imemhukumu kifungo cha miaka 10 jela mwanaume mmoja ambaye alirusha kilipuzi kilichotengenezwa kwa mikono karibu na Waziri Mkuu wa wakati huo Kishida Fumio.
Kimura Ryuji alishtakiwa kwa kuwajeruhi watu wawili aliporusha kilipuzi. Kishida alikuwa akitembelea bandari katika mji wa Wakayama mnamo Aprili 2023 ili kufanya kampeni kwa mgombea katika uchaguzi mdogo wa Baraza la chini la Bunge.
Kimura mwenye umri wa miaka 25 alisimama katika Mahakama ya Eneo la Wakayama kwa mashtaka matano, likiwemo la kujaribu kuua na ukiukaji wa Sheria ya Kudhibiti Vilipuzi.
Ikiwa mshtakiwa alikuwa na nia ya kuua ilikuwa hoja kuu iliyobishaniwa mahakamani hapo.
Waendesha mashtaka walitaka kifungo cha miaka 15 jela, wakidai kuwa Kimura alifahamu kuwa kilipuzi kilikuwa chenye kusababisha vifo. Waliita kitendo chake kuwa kitendo cha kigaidi, kumlenga waziri mkuu aliye madarakani.
Mawakili wa Kimura walitaka kifungo cha miaka 3, wakidai kuwa alitengeneza kilipuzi ili kupata umaarufu na hakuwa na nia ya kuua.