Mwanzilishi wa mtandao wa Telegram Pavel Durov, amefunguliwa rasmi mashtaka kwa makosa ya kushindwa kudhibiti ujumbe hasi unaotumwa kwenye mtandao wake.
Durov lakini ameachiliwa kwa dhamana na yuko chini ya uangalizi mkali wa mahakama.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na mwendesha mashtaka wa mji wa Paris, Laure Beccuau, Durov alitoa dhamana ya euro milioni 5, na atakuwa na wajibu wa kuripoti katika kituo cha polisi mara mbili kwa wiki, na marufuku ya kuondoka katika ardhi ya Ufaransa.
Bilionea huyo mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Urusi mwenye umri wa miaka 39, alikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Le Bourget, katika mji mkuu wa Ufaransa Jumamosi iliyopita kwa tuhuma za kushindwa kuchukua hatua kudhibiti maudhui hasi kwenye mtandao wake wa kijamii unaotumiwa na watu milioni 900. Kampuni ya Telegram imeyekanusha madai hayo.