Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Paul Makonda anatarajia kuanza ziara ya kikazi mkoani Tanga inayotarajiwa kuanza Januari 20 hadi 22, 2024.
Akizungumza ofisini kwake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, Bw. Selemani Sankwa amesema ziara hiyo ni ya kikazi ambayo itaambatana na kufanya mikutano ya hadhara katika wilaya nne za Pangani, Tanga, Muheza na Korogwe, “Ziara hii tunategemea itaendelea kutuimarisha kama chama kwa kutatua changamoto na kusukuma miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Tanga ili ikamilike kwa wakati, hii itasaidia kufikia lengo letu la kushinda mitaa yote 263, vijiji vyote 775 na vitongoji vyote 4572 vya mkoa wa Tanga kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba, 2024” amesema Sankwa.
Katika hatua nyingine, Bw. Sankwa amesema ziara hiyo itaanza tarehe 20 Januari saa 5 Asubuhi katika wilaya ya Pangani na baadaye saa 8 mchana wilaya ya Tanga Mjini.
Tarehe 21 ataendelea na ziara yake wilaya ya Muheza kuanzia saa 3 Asubuhi na baadaye saa 5 Asubuhi atafanya mkutano mwingine Segera na atahitimisha ziara yake Korogwe majira ya saa 8 mchana siku hiyo hiyo ya Tarehe 21.
Katika ziara hiyo, Mwenezi Makonda anatarajiwa kueleza Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Bw. Sankwa ametoa rai kwa wananchi na wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza Mwenezi Makonda.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mwenezi Makonda kutembelea mkoa wa Tanga na wilaya zake tangu alipoteuliwa Oktoba 22, 2023 akichukua nafasi ya Sophia Mjema.