Mwenge wa uhuru mwaka 2024 leo umeendelea kukimbizwa Mkoani Kagera ambapo unakagua na kuzindua miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Ukiwa Wilayani Ngara umezidua mradi wa maji wa Rusumo unaotekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) ukigharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu za Kitanzania.
Akisoma taarifa ya mradi huo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Ngara Mhandisi Saimon Ndyamkama amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi October mwaka 2020 na umekamilika na kuanza kutoa huduma kuanzia mwezi January mwaka huu 2024 na unahudumia wakazi zaidi ya elfu tano wa kata ya Rusumo huku akiongeza kuwa mradi huo ni ufadhili wa benki ya dunia na umewapunguzia wananchi kufuata maji kwa umbali mrefu ikiwa ni sambamba na kupunguza magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa Godfrey Mzava amewapongeza RUWASA kwa jitihada wanazozionyesha za kusimamia mradi ya maji na kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi.