Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi amesema licha ya kero nyingi za Muungano kupatiwa ufumbuzi lakini hazitakwisha kabisa kwasababu yapo mambo yanayoibuka kulingana na mahitaji na matakwa ya wakati uliopo.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 11,2021 wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari kutoka Tanzania bara na Zanzibar Ikulu visiwani humo huku akitaja akaunti ya pamoja kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zilizopo hivi sasa na ugumu wa kuipatia ufumbuzi.
Hata hivyo alisema katika kero zote zilizopo hivi sasa hakuna inayonyima usingizi.
“Changamoto nyingi zimeshafanyiwa kazi kwakweli mambo yanaenda vizuri tupo kwenye hatua nzuri zaidi, tumeshuhudia hata hivi karibuni zimeondoolewa karibu kero 11 zimebaki saba, lakini niseme tu kwamba changamoto za Muungano hazitafika mwisho kwahiyo matatizo yatakuwa yanaibuka lakini yanashughulikiwa,” alisema Dk Mwinyi
Alitolea mfano wa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa kuwa ni akaunti ya pamoja ambayo fedha zote zinatakiwa ziingizwe kwenye akaunti hiyo kisha zitakuwa zinatolewa gharama za kuendesha nchi na fedha zinazobaki zinagawanywa.