Polisi wa Los Angeles wameripoti kumkamata Mwanamume aliyekuwa amejivisha mavazi ya zimamoto ili kuiba kwenye Nyumba katika eneo lililoathiriwa na moto karibu na Malibu ambapo tukio hilo limetokea wakati moto mkubwa ukiendelea kuharibu mali na kulazimisha Watu zaidi ya 100,000 kuhama makazi yao huko Jijini Los Angeles Nchini Marekani.
Kwa mujibu wa Ripoti za Polisi Mtuhumiwa alikamatwa akionekana akiwa amevaa sare za zimamoto, lakini baadaye ilibainika kuwa alikuwa akijaribu kutumia njia hiyo kuingia na kupora Nyumba za Wahanga.
“Tulimkuta akiwa ameketi chini, tukidhani ni mzima moto lakini uchunguzi wa haraka ulibaini kuwa alikuwa ameshiriki katika wizi wa mali ya waathirika,” alisema afisa mmoja wa Polisi.
Aidha Polisi wamesema kuwa Mtuhumiwa huyo alikuwa sehemu ya kundi la Watu watatu waliokuwa wakizunguka maeneo yaliyoharibiwa na moto wakitafuta fursa ya kuiba ambapo pia Polisi wameonya kuwa Mtu yeyote atakayepatikana akijaribu kujipenyeza katika maeneo yaliyoathiriwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Moto huo umeharibu zaidi ya majengo 12,000, ikiwa ni pamoja na mamia ya Nyumba na kusababisha vifo vya Watu 16 huku wengine wakiwa hawajulikani walipo pia Serikali ya jiji imeweka zuio la kutembea usiku katika maeneo yaliyoathiriwa ili kuzuia matukio kama haya, huku adhabu kwa makosa ya kujifanya mzima moto ikitajwa kuwa kifungo cha mwaka mmoja jela.