Michezo

Hizi ndio sababu za Kocha wa Simba kutomchezesha Mwombeki

on

loga_mwomSTRAIKA wa Simba, Betram Mwombeki amekuwa akikumbana na wakati mgumu wa kupata namba katika siku za karibuni ndani ya kikosi cha Msimbazi, zimeelezwa sababu mbalimbali.

Kati ya sababu za hivi karibuni za Kocha Zdravko Logarusic ni kwamba, mchezaji kama hayupo fiti, anashindwa kuendana na kasi ya fowadi yake na wiki moja iliyopita ikaelezwa kwamba ni majeruhi amepewa wiki moja ya kujiuguza na nyingine ya kupumzika.

Lakini Logarusic ametoa nyingine kali ya fowadi huyo mrefu. Anasema kwamba hakumchezesha kwenye mechi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting kutokana na hali ya hewa ndani ya Uwanja wa Taifa ambayo haiendani na mwili wake mkubwa.

Kocha huyo alimnyanyua kwenye benchi Mwombeki ili aingie kucheza zikiwa zimebaki dakika mbili za nyongeza ambazo pia zilimalizika akiwa katika harakati za kuingia katika meza ya mwamuzi wa akiba na hakufanikiwa kuingia.

Alipoulizwa na Mwanaspoti kwanini alifanya hivyo, Logarusic alisema, alimnyanyua dakika hizo za mwishoni na siyo mwanzoni kwa sababu hali ya Uwanja wa Taifa haikustahili Mwombeki acheze. Siku hiyo ilinyesha mvua na kufanya nyasi kuwa na unyevu.

“Unajua Mwombeki ana mwili mkubwa na hali ya uwanja haikuwa nzuri kama ulivyoona mvua ilinyesha wakati wote na nyasi zilikuwa nzito, kutokana na hali ile ilikuwa inawafaa wachezaji wenye miili midogo na siyo wenye miili mikubwa kama Mwombeki na ndiyo maana nilimwacha nje.

“Mwombeki atacheza, ni mchezaji mzuri na atacheza bado tuna mechi nyingi, lakini kwa hali ile ya uwanja kwenye mchezo ule isingemfaa kabisa,” alisema Logarusic.

Alipoulizwa Mwombeki kuhusu hali hiyo alisema: “Siwezi kuzungumzia hilo na sifahamu lolote, chochote kwangu poa.”

Mshambuliaji huyo alikaa kwenye benchi la timu hiyo akiwa na wenzake, Henry Joseph, Abdulhalim Humud, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Edward Christopher, William Lucian ‘Gallas’ na Abuu Hashimu.

Mechi alizozikosa Mwombeki ni dhidi ya JKT Oljoro , Mtibwa Sugar, Mgambo JKT, Mbeya City na JKT Ruvu. Alianzia benchi katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting juzi Jumapili.

Jumapili wiki hii Simba itacheza na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

SOURCE: MWANASPOTI

 

Tupia Comments