Mzee wa Makamo aliyefahamika kwa Jina la Bujukano lusano(75) Mkazi wa kijiji cha Kibanga Wilayani Mbogwe Mkoani Geita, amepandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu Kanda ya Geita kwa kosa la kuua mkewe bila kukusudia.
Shauri hilo namba 29166/2024 linadai mtuhumiwa anashtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha sheria namba 195(1) na 198 cha Kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka ya 2022.
Kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali na Mwendesha mashtaka wa Serikali Scolastica Teffe ambaye ameieleza Mahakama kuwa, Februari 28,2024 huko katika kijiji cha Kabanga mtuhumiwa Bujukano alimuua bila kukusudia mkewe Maria Masalu.
Teffe ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio mshtakiwa alitumia fimbo kumpiga Marehemu akiwa amelala chini maeneo ya kichwani na mgongoni kitendo kilichomsababisha kifo chake mwanamke huyo.
“Taarifa za uchunguzi wa mwili wa marehemu ulionyesha kifo cha marehemu kilisababishwa na majeraha”Mwendesha Mashtaka wa Serikali Teffe.
Wakili huyo wa Serikali ameeleza kuwa katika kesi hiyo watakua na mashahidi tisa na vielelezo viwili .
Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo Jaji anaesikiliza kesi hiyo Kelvin Mhina ameahirisha shauri hilo hadi wakati mwingine litakapopangwa kwa ajili ya usikilizwaji.