Siku kadhaa zimepita tangu Mzee Francis Kanyasu maarufu kama Ngosha ambaye amefariki, kuandikwa na vyombo vya habari kuwa alibuni na kuchora Nembo ya Taifa.
Baada ya hapo ilijitokeza familia nyingine ikidai mzee wao ndiye mchoraji…sasa ili kusitokee mkanganyiko kama huu tumeona ni vyema tukaujua ukweli kupitia kwa wenye kumbukumbu hizi.
Ayo TV na millardayo.com zimekutana na Elias Jengo ambaye ni Profesa Mshiriki Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akifundisha Historia ya Sanaa na Kuchora ambaye anatueleza: “Kumbukumbu yangu ni kwamba kwenye miaka ya 90 hivi nilikuwa Zanzibar nikaonana na Iddi Farhan – mtoto wa Abdallah Farhan. Abdallah Farhan msanii mashuhuri sana…”
Aidha, Profesa Jengo anabainisha kuwa ipo michoro ambayo mzee Abdallah Farhan ameiacha ambayo inaonesha kuwa yeye ndiye alichora Nembo ya Taifa ambayo aliiona kupitia kwa Iddi Farhan: “Akanionesha kazi za baba yake, nikamwambia hii michoro yote mpaka Nembo hii ya Taifa ni kazi ya mzee? Akasema ‘ndiyo hii ni kazi ya mzee. Baba yangu ndiye aliyefanya kazi hii.’ Kwa hiyo, mimi nafundisha wanafunzi wangu kwamba mchoraji wa kwanza wa Nembo ya Taifa katika Tanzania ni mzee Abdallah Farhan.” – Prof. Jengo.
Hata hivyo Profesa Jengo anasema utata upo pale ambapo haijabainika mzee Abdallah Farhan alichora Nembo ipi kwa sababu zipo mbili: “Ziko Nembo mbili – Nembo ya Uhuru wa Tanzania mwaka 1961 mpaka 1964 na ya Muungano tangu 1964 mpaka leo. Ziko Nembo mbili tofauti. Je, Abdallah Farhan alichora zote mbili, ama hii ya Muungano?” – Prof. Jengo.
Ayo TV na millardayo.com zitaendelea kufuatilia kwa wenye kumbukumbu zaidi…
Kwenye video hii yapo mengi ambayo Profesa Jengo ameyaeleza kuhusu nani alibuni na kuchora Nembo ya Taifa na unaweza kutazama kwa kubonyeza PLAY…
Kabla ya kifo chake akiwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili Mzee Francis Kanyasu ‘Ngosha’ aliwahi kukaririwa na Vyombo vya Habari akisema yeye ndiye aliyebuni na kuchora Nembo ya Taifa…hii video ni baada ya kusambaa kwa taarifa hizo ambapo Serikali kupitia Wizara ya Afya ilimhamishia Muhimbili kwa matibabu zaidi…