Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amewataka wasanii wa filamu nchini watembelee Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ili wapate maudhui yatakayowawezesha kuandaa filamu za kuenzi mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika hususani nchi za kusini mwa Afrika.
Hamis Mwinjuma ameyasema hayo leo March 11, 2023 alipotembelea kituo hicho kilichopo Jiji Dar es salaam kwa lengo la kufahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo hicho.
Aidha amekitaka kituo hicho kiharakishe mchakato wa somo la historia ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika kuingizwa katika mtaala wa elimu ili wanafunzi wajifunze na kufahamu mchango wa Tanzania katika harakati za kupigania uhuru ndani ya Bara la Afrika.
Mwinjuma amewahimiza Kituo hicho kuendelea kutekeleza mkakati wa kuanzishwa kwa uhifadhi wa historia ya urithi wa ukombozi kwa njia ya kidijitali ili kurahisisha utoaji wa elimu kwa umma bila kulazimika kufika katika kituo husika.