Naibu Waziri wa Nishati, mh Judith Kapinga, amewataka viongozi wa Mamlaka ya udhibiti Mkondo wa juu wa Petroli (PURA), kuongeza juhudi na ufanisi katika majukumu Yao, ili kuvutia wawekezaji watakaosaidia kuboresha sekta hiyo.
Ameyasema hayo alipokuwa Mkoani Morogoro, wakati akifungua kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa baraza la wafanyakazi PURA, cha kujadili bajeti ya mwaka 2025/26, ambapo amewapongeza na kuwataka viongozi wa taasisi hiyo, kutenda haki wakati wakutimiza majukum Yao.
Akieleza mafanikio ya taasisi hiyo, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya udhibiti Mkondo wa juu wa Petroli na Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema kuwa wamefanikiwa kukamilisha mapitio ya mikataba, kuimarika kwa usimamizi na udhibiti wa mkondo wa gesi asilia nchini, pamoja na kuimarika kwa shughuli za kaguzi na gharama.
Aidha PURA kwa kushirikiana na taasisi nyingine za utafiti wamefanikiwa kugundua gesi kwenye kina cha bahari na sasa mpango ni kuweza kuitengenezea mradi na kuibadili kuwa katika hali ya kimiminika na kuiuza nje ya nchi
Mkakati huo unatajwa kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta hiyo na kuvutia wawekezaji kupitia mnada wa uuzaji wa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, na wanatarajia kunadi jumla ya vitalu 26
Sambamba na hayo, Mhandisi Sangweni amesema kuwa, taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ambapo ni pamoja na ukosefu wa fursa ya kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa wafanyakazi wa PURA kutokana na ukosefu wa fedha ambazo zitakidhi gharama za masomo.