Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewatahadharisha Watumishi wa Umma kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kwa jina la “Kausha Damu” huku akisisitiza kuwa mikopo ya aina hiyo imekuwa ikidhalilisha na kutweza utu wa Watumishi katika Jamii.
Kikwete ametoa tahadhari hiyo wakati akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya Busega Mkoani Simiyu wakati akihitimisha ziara yake Mkoani humo ambapo amesema mikopo hiyo imewafanya baadhi ya Watumishi kuathirika kisaikolojia na kushindwa kufika katika vituo vya kazi na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.
Ridhiwani amesema mikopo hiyo ambayo huchukuliwa kwenye Taasisi za Kifedha zisizotambulika imekuwa na riba kubwa ambayo huwapelekea Watumishi kushindwa kuwasilisha marejesho na kupelekea kuuzwa kwa nyumba au vitu vya thamani wanavyovimiliki hivyo amewataka Watumishi kuanza kutumia Mfumo mpya wa kieletroniki wa kukopa (e-loans) ulioanza kutumika kuanzia Sept 1, 2023 ambao unamuwezesha Mtumishi kuomba mkopo pasipo kufika kwenye Taasisi ya Kifedha au Tawi la Benki.
Amesema mfumo huo umeanzishwa na Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Utawala Bora ili kumsaidia Mtumishi wa Umma kupata mikopo katika Taasisi za Kifedha zinazotambulika na Mwajiri ili kumuepusha Mtumishi kukopa sehemu ambazo humpeleka Mtumishi kunyang’anywa kadi ya Benki.