Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amezindua rasmi matumizi ya mfumo wa teknolojia inayotumika kuboresha utoaji wa huduma za afya (Afya-Tek) ndani ya Mfumo Jumuishi wa Kidigitali wa Afya ngazi ya jamii.
Hafla hiyo ilifanyika Desemba 10, 2024 Kibaha mkoani Pwani na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon John, wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wakiwemo wataalam wa teknolojia, wawakilishi wa mashirika ya maendeleo na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Aidha, Dkt. Mollel amesisitiza umuhimu wa mfumo huu wa kidigitali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi akibainisha kuwa mfumo wa Afya- Tek utaimarisha uratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii, kuongeza uwazi, na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati.
“Mfumo huu unaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya. Unatupa uwezo wa kufuatilia, kupanga, na kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote, hususan wale wa vijijini. Ni hatua muhimu katika kufanikisha azma yetu ya kuwa na afya kwenye kiganja cha mkono kupitia teknolojia,” amesema Dkt. Mollel.
Pia, amesema kuwa, Mfumo wa Afya-Tek umeunganishwa na mifumo mingine ya kidigitali nchini, hatua inayotekeleza agizo la Rais la kuhakikisha mifumo yote ya kidigitali inasomana kwa ufanisi. Hadi sasa, asilimia 80 ya mifumo hiyo imeunganishwa, na Serikali inalenga kufikia asilimia 100 katika kipindi kifupi kijacho.