Namibia imemchagua rais wake wa kwanza mwanamke, Netumbo Nandi-Ndaitwah, 72, makamu wa rais wa sasa kutoka chama tawala, tume ya uchaguzi imetangaza siku ya Jumanne jioni, Desemba 3.
Makamu wa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah, kwa jina la utani “NNN”, mgombea wa chama cha SWAPO ambacho kimetawala nchi hii yenye utajiri wa madini tangu uhuru wake miaka 34 iliyopita, amechaguliwa katika duru ya kwanza kwa 57.31% ya kura, tume ya uchaguzi imetangaza.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Independent Patriots for Change (IPC), Panduleni Itula, 67, anakuja nyuma kwa asilimia 25.50 tu ya kura, kulingana na matokeo yaliyotangazwa siku ya Jumanne jioni na tume ya uchaguzi.
Katika hotuba yake ya kutoa shukrani, Netumbo Nandi-Ndaitwah ameahidi kutimiza ahadi zake, haswa kuunda nafasi za kazi 250,000 katika miaka mitano. Katika nchi hii yenye wakazi milioni tatu, ukosefu wa ajira huathiri karibu nusu ya vijana, kulingana na takwimu rasmi za hivi punde za mwaka 2018.