Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kwanza la wanawake na teknolojia litakalofanyika nchini Machi 7 jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo linalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika teknolojia kutokana na ukweli kwamba maendeleo hayawezi kutenganishwa na teknolojia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Lunchpad ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo, Caro Ndossi amesema wanalenga kuwaleta pamoja wataalamu wa sekta mbalimbali ili kujadili maendeleo ya teknolojia na athari zake kwa wanawake.
“Kwa kasi ya maendeleo ya kiteknolojia, ni muhimu kwamba wanawake wapewe fursa sawa za kuchangia na kuunda mustakabali wa teknolojia. Hivyo basi mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo hatua muhimu kwa wanawake na teknolojia, ukuaji wa teknolojia kama fursa kwa wanawake, teknolojia na ubunifu wa kujumuisha na usawa wa kijinsia,”
Pamoja na mijadala, Caro ameeleza kuwa kongamano hilo litatoa fursa kwa wanawake kuonyesha kazi zao, kubadilishana uzoefu wao na kuungana na wengine katika masuala ya teknolojia.
“Tutaandaa maonyesho ya bidhaa za kidijitali ziilizoundwa kwa ajili ya wanawake na zile zilizobuniwa na wanawake pamoja na programu tofauti, tafiti za kifani kuhusu athari za teknolojia kwa wanawake nchinii,”amesema Caro.
Kwa upande wake Faith Manangwa aliyewakilisha Buni Hub kitengo kilichopo chini ya Tume ya Sayansi Tanzani (Costech) amesema kongamano hilo litakwenda kuibua mjadala mpya wa ushiriki wa wanawake kwenye teknolojia.