Mbunge wa Jimbo la Butiama (MB), Jumanne Abdallah Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amewataka wananchi wa jimbo lake la Butiama kuondoa hofu kuhusu Mto Mara uliokuwa unasadikika kuwa na sumu.
Akizungumza na Wananchi wa jimbo lake la Butiama aliwaomba kuamini taarifa iliyotolewa na Kamati Maalumu ya Kitaifa iliyoundwa na Serikali kuchunguza mabadiliko ya maji ndani ya Mto Mara iliyotoa taarifa kwamba chanzo cha mabadiliko katika mto huo ni shuguli za binadamu pamoja na nguvu za asili.
“Jambo hili Serikali imetuondolea hofu tuamini kwamba tuko salama, Nasisitiza hakuna serikali duniani inapanga kuua raia wake, tahadhari zote zilizotolewa ilikuwa ni kujiridhisha na tuhuma hizo. Mto Mara upo salama mnaweza kuendelea kutumia,” alisema.
Mbunge Sagini aliyasema hayo wakati wa mikutano na wananchi wa Kijji cha Wegero, Kijiji cha Buswahili, Kijiji cha Kirumi, Kijiji cha Kitasakwa na Kijiji cha Kwisero vilivyopo katika Wilaya ya Butiama baada ya kutembelea sehemu za mto huo Serikali zilizoathiriwa kwenye jimbo lake la Butiama ikiwa ni moja ya ziara yake Mkoani Mara.
Aidha, aliwauliza wananchi hao kama kuna madhara makubwa yaliyotokea kwa mifugo yao baada ya kutumia maji ya mto huo na kuwaeleza kuwa kama mto huo ulikuwa una sumu basi ni lazima mifugo ingedhurika.