Akizungumza wakati akiikaribisha Timu ya Wataalamu kutoka Taasisi hiyo Jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema tathimini hiyo ni fursa kwa Tanzania kuweza kuyafikia Masoko ya fedha ya Kimataifa yatakayoiwezesha Nchi kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi.
Dkt. Mchemba amesema kuwa tathimini huru inayofanywa na Taasisi hiyo itaiwezesha Tanzania kuaminiwa na Taasisi za fedha za kimataifa hivyo kuchochea uwekezaji ambao utakuza uchumi wa Nchi pamoja na ajira kwa Vijana na kwamba ujio wa Wataalamu hao unajibu kiu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza Nchi ifanyiwe tathimini ili kubaini uwezo wake wa kuyafikia masoko ya fedha ya kimataifa katika kuharakisha maendeleo ya Watu.