NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema baada ya kupata uhuru mwaka 1960, Nchi za Afrika zimepiga hatua kubwa katika kuzalisha na kusambaza umeme kwa wananchi wao.
Dk. Biteko amesema hayo leo Januari 27 kwenye Mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ‘Mission 300’ unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam
Naibu Waziri Mkuu amesema lengo kuu la mkutano huo kuitishwa ni kufikia lengo la kuongeza upatatikanaji wa umeme kwa angalau watu milioni 300 barani Afrika katika miaka mitano ijayo
“Inasikitisha kwamba idadi ya Waafrika ambao hawana umeme inakadiriwa kuwa milioni 571.kutokana na hali hii, Mkutano huu uliitishwa, ukiwa na lengo kubwa lakini linaloweza kufikiwa la kuongeza upatikanaji wa umeme kwa angalau watu milioni 300 barani Afrika katika miaka mitano ijayo,” amesema kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine, amesema ili kuunga mkono mpango wa Mission 300 Mikataba ya Kitaifa ya Nishati iliyobuniwa na nchi kumi na nne (14) za majaribio itatoa mfumo wa hatua zilizoratibiwa ili kufungua uwekezaji wa ziada kutoka kwa serikali, washirika wa maendeleo, wahisani, na sekta binafsi katika kufikia malengo ya upatikanaji wa nishati.
Mkutano huo ni mwendelezo wa matunda ya diplomasia ya Tanzania ambapo Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kutangazika barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki katika Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) uliofanyika Brazil Novemba 2024 na Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) na kupewa na nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya Bara la Afrika ni kielelezo cha diplomasia ya Tanzania kuimarika duniani.