Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community-SADC) zimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake katika usimamizi na uhifadhi wa misitu miombo hasa katika kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kuelekea nishati safi ifikapo mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 18,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika Mkutano wa Kimataifa unaohusu Misitu ya Miombo jijini Washington DC nchini Marekani.
“Kikubwa nchi zimeweza kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akitoa maelekezo mbalimbali kwetu sisi kama Wizara na Sekta katika kuhakikisha kwamba misitu ya miombo inalindwa kwa nguvu kubwa, na kwa namna ambavyo amechukua uamuzi thabiti wa kuhakikisha kwamba inapofika mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80 ya wananchi watakuwa wameachana na matumizi wa kuni na mkaa na watakuwa wamejielekeza katika nishati safi ya kupikia” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amesema kuwa misitu ya miombo nchini Tanzania na katika ukanda wa kusini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa misitu ambao unasababishwa na ukataji wa miti usiozingatia sheria, taratibu na kanuni, moto, kilimo cha kuhamahama, uharibifu wa vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, amefafanua kuwa kupitia mkutano huo, wadau mbalimbali wameanza kuonesha nia ya kusaidia mpango wa utekelezaji wa Azimio la Maputo la mwaka 2022 kuhusu ulinzi na uendelezaji wa misitu ya miombo.
Amesema lengo la Mkutano huo ni kuona namna ya kuendeleza Azimio la Maputo katika kulinda na kuendeleza Misitu ya Miombo ambapo takribani asilimia 93 ya misitu ya Tanzania ni miombo ambayo pamoja na mambo mengine, inatunza wanyamapori , vyanzo vya maji na huduma nyingine za kijamii.