Msanii kutoka kiwanda cha filamu Tanzania Rose Ndauka amekuja na kampeni ya usafi maalun kwa ajili ya kuliweka safi jiji la Dar es salaam na wilaya zake ambayo ameipa jina la Ng’arisha Tanzania ambayo anategemea kuianza Jumamosi ya March 15.
Kampeni ya Ng’arisha Tanzania inahamasisha kuweka mazingira ya jiji katika hali ya usafi na kupendeza na pia kutunza mazingira,Kampeni hii itahusisha kufagia baadhi ya mitaa katika manispaa ya Ilala,kuzoa taka na kuzitupa maeneo husika au kuziteketeza.
Kwa kuwa jukumu la usafi katika miji linafanywa na mamlaka husika lakini pia kufanya usafi ni jukumu la kila raia hasa katika maeneo tunayoishi na kufanyia shughuli zetu za maisha pia ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa hatuwi chanzo cha kuweka miji katika hali chafu.
Kutokana na hayo Rose Ndauka kama msanii wa filamu na akiwa kama kioo cha jamii ameamua kuwashirikisha viongozi,raia wa kada mbalimbali na mamlaka husika kuendesha kampeni hii ya Ng’arisha Tanzania siku ya Jumamosi tarehe 15 Machi 2014,kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 5 asubuhi.
Wasanii wenzake waliothibitisha kuwepo kwenye kampeni hiyo mpaka sasa ni pamoja na Monalisa,Yusuph Mlela,Slim Omary,Riyamma Ally na wengine wengi.