Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Wazazi na Walezi kuwalea Watoto na Vijana kwa kuzingatia maadili ya kitanzania pamoja na kuongeza umakini katika maudhui yanayooneshwa katika Televisheni.
Dr. Mpango ameyasema haya wakati akiongea na Waumini wa Kijiji cha Kasumo Mkoani Kigoma baada ya kushiriki Ibada ya kawaida ya katikati ya wiki katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani Kijiji hapo ambapo
amesema kumekuwepo na mmomonyoko wa maadili ikiwemo ndoa za jinsia moja ambazo hazipo hata kwa Wanyama hivyo Wazazi waangalie Watoto na Vijana wanaangalia nini ili kuondokana na kuwa na Taifa la ajabu.
“Hili ni gumu kweli, maadili ya Nchi yetu yameporomoka sana, yaani na mengine hata kuyasema ni ngumu, ndoa za Wanaume wawili?, ndoa za Wanawake wawili? mliziona wapi? hata Wanyama hawafanyi hivi”
Kwa upande mwingine, Dr. Mpango amewaasa Wananchi wa Kasumo na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla kutoa ushirikiano wakati huu ambapo Serikali inafanya ujenzi wa miundombinu ya Barabara katika Mkoa huo ambao ni nyenzo muhimu kwa biashara na urahisi wa kufikia huduma za jamii kama vile Hospitali na Shule na kuzingatia pia kuwapa Wawekezaji ushirikiano ikiwemo kuzingatia bei halisi za ardhi katika maeneo yao ili kutowapoteza.