Mbunge wa Kigamboni Dkt Faustine Ndugulile (Mb) ameliomba Bunge kupitisha azimio la kubinafsisha huduma za vivuko nchini.
Dkt Ndugulile aliyasema haya wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyowasilishwa mapema Bungeni, Dodoma.
Dkt Ndugulile amedai kuwa Taasisi ya Temesa imeshindwa kusimamia na kuendesha huduma za vivuko Kigamboni, hali inayopelekea kuwepo kwa malalamiko ya mara kwa mara toka kwa wakazi wa Kigamboni wanaotumia huduma hii.
Dkt Ndugulile ameitaka Serikali kuchukua hatua stahiki na kutosubiri maafa kabla ya kuchukua hatua.
Aidha, Dkt Ndugulile ameiomba Serikali kufanya mapitio ya zabuni ya ukarabati wa MV Magogoni ambayo inatarajiwa kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya ukarabati. Dkt Ndugulile amesema kuna taasisi nchini zenye uwezo wa kukarabati na kujenga meli ndogo ndogo. Hivyo, kufanya ukarabati wa MV Magogoni nje ya nchi, utapelekea kufanya malipo kwa fedha za kigeni na kuathiri ajira ambazo zingetumika kwenye ukarabati huo.