Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili leo January 07,2024 Jijini Dar es salaam ambapo jumla ya Wanafunzi 592,741 kati ya 694,769 wenye matokeo ambao ni sawa na 85.31% wamefaulu ambapo wamepata madaraja ya I, II, III na IV.
“Mwaka 2022 Wanafunzi waliofaulu walikuwa 539,645 sawa na 85.18% , hivyo kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa 0.13% pamoja na ongezeko la idadi ya Wanafunzi 53,096 sawa na 9.84% ya Wanafunzi waliopata fursa ya kuendelea na kidato cha tatu ikilinganishwa na mwaka 2022”
“Kati ya Wanafunzi waliofaulu kuendelea na kidato cha tatu, Wasichana ni 314,949 sawa na asilimia 83.66 na Wavulana ni 277,792 sawa na 87.28%, takwimu zinaonesha kuwa, Wavulana wamefaulu vizuri ikilinganishwa na Wasichana”
NECTA imetangaza pia matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne uliofanyika mwaka 2023 ambapo jumla ya Wanafunzi 1,287,934 kati ya 1,545,330 wenye matokeo sawa na asilimia 83.34 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B, C na D.(Swipe kwa matokeo ya darasa la nne).