Kuelekea maadhimisho ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Aprili 8 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua kauli mbiu inayosena “MIAKA 60 YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TUMESHIKAMANA NA TUMEIMARIKA, KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU’’ pamoja na Nembo maalum itakayoenda kutumika katika maadhimisho hayo yatakayofanyika Aprili 26 katika uwanja wa uhuru Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Jijini Dodoma Waziri mkuu amesema Muungano huo umeendelea kuwa na tija na kuchagiza maendeleo ya nchi na wananchi wote kwa ujumla.
“Kauli mbiu hii inatukumbusha kuwa Muungano wetu umekuwa kichocheo cha maendeleo kwa pande zote mbili za muungano, hakuna mwananchi ambaye hajafikiwa na faida za muungano wetu, ama kwa hakika Muungano wetu ni wa udugu, wananchi wengi wameunganisha udugu, urafiki na wengine wameoleana,”amesema.
Amesema pamoja na misingi ya kisiasa, hakuna anayeweza kuvunja udugu wa damu uliopo, Udongo ulianza kuchanganywa sasa kuna mchanganyiko mkubwa wa damu.
Pia amezitaka taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano kuanzia elimu ya awali ili watoto na vijana waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika kuundeleza Muungano huo.
Aidha amesema uzinduzi huo wa Nembo na kaulimbiu ya Miaka 60 ni moja ya sehemu ya maadhimisho ambapo mwaka huu yamepambwa na matukio mengine muhimu ikiwemo uchaguzi wa wenyeviti wa mitaa hivyo amewaomba wananchi kuchagua viongozi wenye weledi na watakaoweza kudumisha Muungano.