JAMBOLEO
Mtoto mwenye umri wa miaka 13 amekamatwa usiku akiwa uchi kwa madai kuwa alikuwa akiwanga katika duka moja lililopo kijiji cha mpunguti Mkoa wa Mbeya.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa mtoto huyo ni mzoefu kwa kuwa wafanyabiashara wamekuwa wakipotelewa na fedha katika amzingira ya utata ambapo walitenga mtego ili kubaini upotevu huona kumbaini akiingia kwenye duka moja ambalo linadaiwa kuzindikwa.
Taarifa za awali kutoka kwa wakazi wa eneo hilo walidai taarifa za mtoto huyo ambaye alikuwa anaishi na bibi yake aliyemfukuza kutokana na tuhuma za ushirikiana na kukimbilia msituni kutokana na kukosa pa kuishi.
Inasemekana motto huyo aliishi misituni kwa zaidi ya miezi mitano ndipo aliporejea na kuolewa lakini ndoa yake haikudumu kutokana na maisha kuwa magumu na akaamua kuanza mbinu za kichawi kwa kuibia watu.
Alianza kufungua kufuli za maduka kwa kutumia kidole gumba huku akiwa uchi na alinaswa na kupelekwa kwenye ofisi za kata ambapo anashikiliwa hadi sasa.
NIPASHE
Mwanamke mmoja ambaye alimpiga kichwani rais Nicolas Maduro kwa embe ameahidiwa nyumba mpya kutokana na matatizo yanayomkabili kufuatia tukio hilo la aina yake nchini Venezuela.
Rais huyo mwenye miaka 52 alikuwa akienda basi kupitia kwenye kundi la watuwiki moja iliyopita kwenye moja ya majimbo nchini humo na ndipo mtu mmoja katikati ya watu hao alipotupa tunda hilo na kumpata.
“Marleny Olivo alikuwa na tatizo la nyumba yake, na walimuita lakini mwanamke huyo aliogopa na hakuamini kama ilikuwa ni kweli,Nimeidhinisha nyumba kwa ajili yako kama sehemu ya misheni ya ujenzi wa nyumba nchini Venezuela” alisema rais huyo MADURO huku akiapa kulila embe alilorushiwa na mwanamke huyo.
Tukio hilo limevuta hisia ya watu wengi kwenye mitandao ya kijamii nchini humo huku likiambatana na utani kila wakati.
NIPASHE
Watanzania waliokuwa wanaishi nchini Afrika kusini jana wamerejeshwa nchini kufuatia mashambulizi ya wazawa dhidi ya wageni yanayoendelea nchini humo.
Kundi hilo liliwasili jana majira ya saa 11 alfajiri katika uwanja wa ndege na shirika la ndege la Fastjet.
Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha Serikali kupitia Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa kilisema watanzania hao walikuwa wakiishi katika kambi ya dharura nchini humo.
Walisindikizwa kurudi nchini na ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Elibahati Lowassa na zoezi lilisimamiwa na kuratibiwa na Ubalozi.
MWANANCHI
Wakati viongozi wajuu wa CCM wakiendelea kulalamikia makada wanaowatuhumu kutumia fedha kujifagilia njia ya urais, mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amesema taasisi yake inakusanya taarifa zote za wanachama wa chama hicho tawala wanaotuhumiwa kutumia mlungula.
Mara kadhaa viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakiwaonya wanachama wao dhidi ya makada wanaotumia fedha kujitengenezea mazingira mazuri ya kupitishwa na chama hicho kugombea urais, lakini wameeleza kuwa hawawajibiki kuwaripoti Takukuru kwa kuwa ni wajibu wa chombo hicho cha kuzuia na kupambana na rushwa kufanyia kazi malalamiko hayo.
Jumatano, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema Takukuru hawahitaji kupata mwaliko wa CCM ili kufanya uchunguzi wa kukamata wagombea wanaotumia rushwa ndani ya chama hicho kwani rushwa inayoendelea kwa sasa iko wazi.
“Kazi ya kuwafuatilia imeshaanza muda mrefu, tunazo taarifa zao za kutosha kwa kila mwanasiasa anayelalamikiwa,” Dk Hoseah
Dk Hoseah alisema kwa muda mrefu Takukuru imekuwa ikifuatilia mienendo ya wanasiasa wanaotaka uongozi kupitia chama hicho na ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema Takukuru kwa sasa inaendelea na kazi yake ya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo huku ikikusanya taarifa za kila mwanasiasa anayeonekana kutuhumiwa na vitendo vya rushwa.
“Siyo kwamba Takukuru haijaona wala haisikii malalamiko ya viongozi CCM. Tunajua wajibu wetu na kazi ya kuwafuatilia imeshaanza,” Dk Hoseah.
“Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 imekataza wazi kwamba, ni makosa kutoa chochote kama zawadi kwa kundi la watu, vinginevyo ni kukiuka sheria hiyo. Labda kama anaonekana kuwa na fedha nyingi basi ajenge hata barabara kuliko kufanya hivyo.”
Dk Hoseah aliongeza kuwa sheria pia inazuia kuanza kampeni kabla ya muda kupangwa rasmi na Tume ya Taifa (Nec), kwa hivyo muda wa kampeni utakapoanza, itarahisisha kukusanya taarifa zake na kuchukua hatua kwa wanasiasa hao.
MWANANCHI
Balozi wa zamani wa Tanzania kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN), Dk Augustine Mahiga amesema anafuatwa na makundi ya watu wanaomshawishi achukue fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM, lakini hajatoa jibu.
Balozi Mahiga anaingia kwenye orodha ya watu ambao wamejitangaza au wanatajwa kuwania nafasi hiyo ya juu kwenye siasa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakaochagua Serikali ya Awamu ya Tano.
Tayari makada 21 wa chama chake wanatajwa kuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake wa miaka 10 baada ya kuongoza nchi kwa vipindi viwili, ambavyo ndio kikomo kwa mujibu wa Katiba.
Tayari makada 21 wa chama chake wanatajwa kuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake wa miaka 10 baada ya kuongoza nchi kwa vipindi viwili, ambavyo ndio kikomo kwa mujibu wa Katiba.
Dk Mahiga, ambaye pia alikuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia, alisema makundi hayo yalianza kumfuata baada ya Rais Kikwete kutangaza kwenye sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika Songea kuwa kama wanachama wanaona kuna mtu anafaa kugombea urais na hajajitokeza, wamfuate na kumshauri achukue fomu.
“Nimepata makundi ya watu na mtu mmoja mmoja wakinishauri nichukue fomu ya kuwania urais baada ya Rais Kikwete kutoa kauli kule Songea mkoani Ruvuma, lakini bado sijakubali wala kukataa ushawishi huo,”
Lakini akaongeza kuwa kushawishiwa kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo nyeti kwa Taifa, ni jambo moja, lakini kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ni jambo jingine akisema kuwa CCM ina mchakato na masharti ambayo ni lazima yatimizwe.
Hata hivyo, Dk Mahiga hakusita kumwaga sera zake iwapo atajitosa kuwania nafasi hiyo na kuchaguliwa kuongoza nchi.
“Nitaimarisha demokrasia, kuongeza uwajibikaji, kuimarisha maadili, kuboresha mwelekeo wa uchumi, kilimo, kuimarisha reli na kupambana na rushwa,” alisema balozi huyo ambaye ni mhitimu wa shahada ya umahiri ya sanaa.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete leo atahudhuria sherehe za mwisho za Muungano na kukagua gwaride la 10 la shughuli hiyo tangu aingie madarakani wakati wa maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano yatakayofanyika kwenye uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam.
Kikwete atahitimisha kipindi chake cha miaka 10 cha kuongoza nchi mwishoni mwa mwaka huu baada ya kupatikana kwa mrithi wa kiti kwenye uchaguzi mkuu ambao kikatiba unatakiwa ufanyike mwishoni mwa Oktoba.
Tayari Kikwete ameshahudhuria sherehe za mwisho za Uhuru akiwa Rais zilizofanyika Desemba 9 mwaka jana.
Sherehe hizo zinafanyika April 26 kila mwaka katika kumbukumbu ya kuunganisha mataifa ya Tanganyika na Zanzibar yaliyoungana mwaka 1964.
MWANANCHI
Serikali imeanza kutimiza ahadi yake ya kuyafuta mashirika na asasi zisizo za kiserikali, NGO, yakiwamo ya kidini na kwa kuanzia imetangaza kusudio la kuzifuta asasi 24 katika kipindi cha siku saba kuanzia jana.
Miongoni mwa asasi hizo ni taasisi mbili za dini ambazo ni Tanzania Muslim Social Community na Tanzania Christian Outreach Ministries ambazo zimepewa siku saba kujitetea.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Issack Nantanga aliliambia gazeti hili kuwa asasi zote zitakazothibitika kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake, zitafutwa.
Nantanga pia alisema panga hilo litazipitia pia asasi ambazo zimekuwa haziwasilishi kwa msajili ada ya kila mwaka na taarifa za fedha zilizokaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa.
“Haya mashirika 24 ndio tumeanza nayo na ukaguzi unaendelea. Tumetoa muda wa siku saba kuanzia leo (jana) kujitetea kwanini yasifutwe na wakishindwa kufanya hivyo, yatafutwa rasmi,” alisema.
Mashirika mengine ni Mbezi Juu and Salasala Woman Agricultural and Environmen Association, Waridi Training Society, Vituka Machimbo Development Association na Gerezani Nguvukazi.
Mengine ni Nyakasangwe Small Scale Farmers Association, Vitendo Trust Fund, Bahari Beach Silvers and Woman Association, Owners Social Club na Magovent Development Association.
Kwa mujibu wa Nantanga, mashirika mengine yaliyomo katika orodha hiyo ni Hananasifu Quarters Women Association, Mburahati Barafu Development Community na The Movers Club.
Pia yamo Umoja wa Maendeleo ya Jamii Mlima Mindu, Tabata Tujiimarishe Club, Umoja wa Wauza Miche Ubungo, Kunguru/Kinzudi Development Association na Women & Environment Association.
“Ukitazama katika tovuti ya wizara utakuta tuna orodha ya mashirika 10,624 yaliyosajiliwa tangu 1953. Tutapitia moja baada ya jingine na yatakayobainika kukiuka sheria yatafutwa,” alisisitiza.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenyeTwitter,Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa>>> TwitterInstaFB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribeYouTube kwa kubonyeza hapa>>>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.