Magazeti

#MAGAZETINI JUNE 03…Mbunge wa Ukonga afariki usingizini, Makada watano kuchukua fomu leo na SITTA avunja bodi ya TPA

on

late

MTANZANIA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), imetakiwa kukunjua kucha zake kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.

Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema sasa umefika wakati kwa Takukuru kuhakikisha wanadhibiti matumizi ya fedha kwa wagombea wanaotangaza nia katika vyama mbalimbali.

Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema ni lazima Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea, aeleze mikakati yake ya namna atakavyopambana na rushwa, hasa kwa wagombea ambao si waadilifu na ambao wamekuwa wakitumia fedha.

“Ni muhimu katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu, Dk. Hosea akaelezea mikakati yake ya kupambana na wanaowania uongozi ambao wanakiuka maadili ili waeleze fedha wanazotumia wanazitoa wapi. Na jambo hili liwe kwa vyama vyote,”Prof. Lipumba.

Akizungumzia uteuzi wa wagombea ubunge na urais kupitia Ukawa, alisema hivi sasa kila chama kipo katika mchakato wa ndani kwa ajili ya kukamilisha taratibu zake.

Ukawa unaendelea vizuri, nami nimetangaza nia ndani ya chama changu kwa nafasi ya urais, nasubiri mkutano mkuu wa chama chetu ndiyo utatoa uamuzi wa mwisho.

“Tukishakamilisha kazi hii kwa kila chama sasa ndiyo kamati maalumu ya viongozi itaketi kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Ukawa na kisha utatoa na jina la mgombea mmoja wa urais ambaye atapambana na vyama vingine,”  Lipumba.

Alizungumzia pia utendaji kazi na weledi wa taasisi za Serikali ikiwamo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ambao walichunguza tukio la kupigwa kwa viongozi na wafuasi wa CUF Januari 27, mwaka huu wakati walipokuwa wanakwenda kuahirisha mkutano wa hadhara.

Ripoti iliyotolewa na tume hiyo, ilieleza kwa kina namna Jeshi la Polisi lilivyotumia nguvu kupita kiasi na hata kusababisha majeruhi kadhaa kinyume cha sheria.

MTANZANIA

Mbunge wa Ukonga jijini Dar es Salaam, Eugen Mwaiposa, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana mjini Dodoma akiwa usingizini.

Akitangaza msiba huo bungeni jana, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Mwaiposa alifariki dunia akiwa nyumbani kwake eneo la Chadulu mjini hapa.

Alisema kwa muda mrefu mbunge huyo aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010, alikuwa na tatizo la shinikizo la damu.

Wabunge walikuwa wakiendelea kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o ambaye ghafla alimkatiza mchangiaji kuzungumza na kumpisha kwenye kiti Naibu Spika Ndugai, ambaye alitoa taarifa za kifo cha mbunge huyo.

Ndugai, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa uchunguzi zaidi wa wataalamu.
Alisema mwili wa marehemu utaagwa kesho mjini hapa baada ya ndugu wa marehemu kuwasili.

Kutokana na msiba huo, Ndugai alitangaza kuahirishwa kwa Bunge hadi keshokutwa na kuagiza Kamati ya Uongozi kukutana na wabunge watapatiwa taarifa kwa njia ya mtandao wa simu.

“Natumia kifungu cha 152 kuahirisha Bunge hadi Alhamisi saa 3:00 asubuhi,” Ndugai.

Mwaiposa ni mbunge wa pili kufariki dunia kwa mwaka huu, akimfuatia Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, aliyefariki dunia Februari 28.

NIPASHE

Makada watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo watafungua pazia kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Leo ndiyo siku ya kwanza ya uchukuaji fomu ndani ya CCM kwa ajili ya kurithi nafasi ya Rais Jakaya Kikwete ambaye anang’atuka kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Makada watakaochukua fomu hizo leo baada ya kutangaza nia kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Charles  Makongoro Nyerere.

Makada hao watatangulia kuchukua fomu hizo huku chama hicho kikitoa masharti makali yanayotakiwa kufuatwa na wagombea.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Idara ya Oganizesheni, Dk. Mohamed Seif Khatibu, alisema makada watano wataanza kufungua pazia la uchukuaji fomu leo katika makao makuu CCM mjini Dodoma.

Alisema katika utaratibu huo, Prof. Mwandosya ndiye atakayekuwa wa kwanza kuchukua fomu saa 4:00 asubuhi akifuatiwa na Wasira.

Dk. Khatibu alisema Lowassa atakuwa wa tatu kuchukua fomu hiyo saa 7:00 mchana, akifuatiwa na Balozi Amina saa 8:30 na Nyerere atafunga dimba kwa leo.

Alisema ratiba ya uchukuaji fomu hiyo haikupangwa kwa kufuata umaarufu au cheo cha mtu ndani ya chama na serikali bali umezingatia mgombea kuwahi kutoa taarifa katika chama kwamba anataka kuchukua fomu.

Kwa upande wa Zanzibar, alisema wagombea wanaowania urais wa Zanzibar watachukulia fomu katika ofisi za CCM na wale wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watachukulia mjini Dodoma.

NIPASHE

Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya  Nchi, Pereira Ame Silima, amesema moja ya mambo ambayo hayakufanyika vizuri mwanzoni wakati wa uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa ni kutovifanya vitumike kupiga kura katika uchaguzi mkuu.

Amesema kama kitambulisho hicho kingeboreshwa kingeweza kutumika kwa ajili ya kupiga kura, hivyo kusingekuwapo uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Waziri huyo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam,  wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa lijulikanalo kama ‘Govetnment Forum on Electronic Identity in Africa’, unaofanyika Afrika kwa mara ya kwanza na kujumuisha wataalam zaidi ya 300 wa ndani na nje ya Afrika.

“Kama tungejipanga mwanzo vizuri ni wazi kusingekuwapo haja ya mchakato unaoendelea wa kuandikisha kwa kutumia BVR, ni nafasi kwetu kujifunza na kujirekebisha na pia watajifunza kutoka Tanzania,”.

Silima alisema siku zijazo vitambulisho hivyo vitaboresha zaidi ili kutumika kwenye maeneo mbalimbali, na kwamba kwa siku za usoni vitatumika kwenye malipo mbalimbali.

Aliwataka Watanzania wanaoshiriki katika kongamano hilo kupokea na kutumia teknolojia inayotoka kwenye makampuni mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu, alisema watu milioni 6.1 wameandikishwa katika maeneo ya Zanzibar, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro na Tanga na kwamba watu milioni 2.5 wamepatiwa vitambulisho.

Alisema kongamano hilo linalojulikana ‘Govetnment Forum on Electronic Identity in Africa’, limeleta pamoja nchi 24 ambazo zitajadili kwa kina changamoto zilizopo kwenye uandikishaji, uandaaji wa vitambulisho vya Taifa na jinsi gani vitatumika kwa maendeleo ya Taifa.

NIPASHE

Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta, amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iliyoundwa na mtangulizi wake, Dk. Harrison Mwakyembe, na kuunda bodi mpya yenye wajumbe wanane kuanzia Juni 2, mwaka huu.

Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa kifungu Namba 6 Kifungu kidogo cha 2 (b) cha Sheria ya Bandari namba 17 ya mwaka 2004 kinachompa mamlaka ya kuvunja na kuteua wajumbe wa bodi.

Sitta alitangaza uteuzi huo jana jijini Tanga wakati wa ziara ya kikazi katika Bandari ya Tanga na baadaye kuzungumza na wafanyakazi waliokusanyika katika uwanja wa Baraka na kusisitiza kuwa mabadiliko hayo yametokana na vitendo vya uonevu alivyokuta vikiendelea kufanywa ndani ya TPA.

“Uteuzi huu unatengua uteuzi wa wajumbe wa sasa wa bodi hiyo kuanzia leo Juni 2, mwaka huu na lengo la uteuzi wa wajumbe hawa ni kuleta tija na ufanisi wa utendaji kazi ndani ya wa Mamlaka na kwa nafasi ya Mwenyekiti mpya wa Bodi nasubiri uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kwani ndiye mwenye mamlaka hiyo kisheria,” alisema.

Dk. Mwakyembe aliteua bodi ya TPA  Novemba 6, 2012.

NIPASHE

Taasisi za serikali zinadaiwa Sh. bilioni 20 na mamlaka za maji nchini.

Hayo yalisemwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Leticia Nyerere.

Mbunge huyo alisema ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara inadaiwa Sh. milioni 102 na Jeshi la Wananchi wa Tanzania linadaiwa Sh. milioni nane na kuhoji kwa nini serikali haiingilii kati ili kuhakikisha kwamba madeni hayo yanalipwa ili kuiwezesha Mamlaka ya Maji ya Musoma (MUWASA) kufanyakazi yao kikamilifu na kwa mafanikio.

Akijibu, Makalla alikiri serikali kutambua kuwapo kwa madeni hayo.

Alisema Jeshi la Wananchi linadaiwa Sh. milioni 2.4, hospitali zinadaiwa Sh. milioni 113 na madeni mengine hivyo mamlaka hiyo inaidai serikali jumla ya Sh. milioni 390 na kwamba mamlaka zote za maji nchini zinaidai taasisi za  serikali Sh. bilioni 20.

“Sisi (Wizara ya Maji) tutashirikiana na Wizara ya Fedha kuona kwamba madeni haya yanalipwa ili mamlaka hizi ziweze kufanyakazi kwa ufanisi,” alisema.

Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere, alitaka kujua kama serikali ipo tayari kutoa ruzuku kwa mamlaka za maji ikiwamo Muwasa ili ziweze kujiendesha na kupunguza mzigo kwa wananchi.

Pia alihoji kama ni sawa wizara na idara za serikali kama JWTZ, Polisi, Ikulu kukatiwa maji kwa kushindwa kulipia huduma hiyo.

Akijibu, Makalla alisema serikali ilianzisha mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini ambazo ziko katika madaraja matatu, ‘A’, ‘B’ na ‘C’.

Alifafanua kuwa mamlaka za daraja ‘B’ ni zile ambazo zinapata ruzuku ya kulipia sehemu ya gharama za umeme wa kuendesha mitambo.

HABARILEO

Watanzania milioni 25.4 wamejitokeza kupima Ukimwi kwa hiari, ikiashiria kwamba nusu ya Watanzania wamepima kujua hali yao kuhusu maambukizi ya Ukimwi.

Idadi hiyo ni ongezeko la watu milioni 4.9 waliopima kufikia Desemba 2013.

Takwimu hizo zimetolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake katika kikao cha 19 cha mkutano wa 20 wa Bunge.

Alisema hadi kufikia Desemba 2014, idadi ya watu waliopima virusi vya Ukimwi (VVU), walikuwa 25,468,564 na kufanya ongezeko la watu 4,999,323.

Kwa mujibu wa Waziri wanaopima VVU kwa hiyari imeongezeka kutoka watu 11,640 mwaka 2009 na kufikia 20,469,241 kwa mwaka 2013.

Alisema mafanikio hayo yametokana na kutekelezwa mpango mkakati wa lll wa sekta ya afya katika kupunguza maambukizi ya Ukimwi.

Alisema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kampeni imefanikiwa kuhamasisha wananchi na pia kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi 5.3 mwaka 2012 .

Alisema pamoja na kuendelea kutekeleza mpango mkakati huo wa tatu wa sekta ya afya wa kupambana na Ukimwi (2013-2017) kwa kutoa ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa hiari, wizara itaendelea kupanua huduma na upimaji kufikia ongezeko la watu 7,411,619 na kutoa dawa za ARV kwa waviu 880,681.

Aidha, alisema kwamba wizara yake imewezesha kliniki 109 zinazotoa ARV kwa wanawake wajawazito wenye VVU (Option B+) ziweze pia kutoa huduma za kupambana na Ukimwi kwa watoto wanaosihi na VVU.

MWANANCHI

Waziri Mkuu  wa zamani, Frederick Sumaye ametangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM, huku akibainisha kuwa amejipima, ametafakari na kujiridhisha kuwa anatosha kushika wadhifa huo wa juu nchini.

“Kama kuna mtu mwingine amekamilika kuliko mimi niambieni na nitampisha (katika mbio za urais),” alisema Sumaye wakati akitatangaza nia hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari, akitumia takriban saa moja na nusu kueleza sifa za Rais ajaye na vipaumbele vyake.

Sumaye, mmoja wa makada sita waliokuwa wamefungiwa na CCM kwa kukiuka taratibu za kampeni, alikuwa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kipindi chote cha miaka kumi na pia alikuwa mbunge wa Hanang hadi alipoamua kutogombea nafasi hiyo mwaka 2010.

Waziri huyo mkuu wa zamani amekuja na kauli mbiu ya Uongozi Bora: Komesha Rushwa, Jenga Uchumi, huku akibainisha vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kujenga na kuimarisha uchumi.

Vipaumbele vingine ni kulinda Muungano, mshikamano, amani na utulivu na kuboresha huduma za kijamii na maisha ya Watanzania, kupambana na maovu ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya, mauaji ya kishirikina, uhusiano wa kimataifa na masuala muhimu ya uhifadhi wa mazingira, kilimo, ajira, ulinzi wa rasilimani na michezo na utamaduni.

Sumaye alisema Watanzania wanataka Rais anayetambua uzito wa kazi iliyopo mbele yake na wananchi wote na awe tayari kuwa Jemedari wa Jeshi hilo ili kupata ufumbuzi wa matatizo yao yanayowakabili.

Alisema wananchi wengi wanamfahamu kwa utendaji wake naye anajua wanachokihitaji na sifa za Rais wanayemhitaji, hivyo yeye ndiye anayefaa kwa nafasi hiyo.

“Mtu anayetaka kuwa Rais ni lazima awe tayari kujipima, kutafakari, ajiridhishe, kuwa anatosha kiafya, kiakili, kimaadili na kidhamira kuwaongoza Watanzania.

“Kama kuna mtu anapungukiwa kimojawapo, hana sifa za kuwaongoza Watanzania,” alisema Sumaye huku akishangiliwa na baadhi ya wafuasi waliomsindikiza katika mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Hyatt Regency.

Alisema kiongozi huyo awe tayari kupimwa na umma vigezo hivyo na siyo ajipime na kwamba yeye yupo tayari kupimwa na umma.

Katika hotuba yake hiyo iliyokuwa ikirushwa na baadhi ya televisheni na redio nchini, alisema Watanzania wanahitaji Rais atakayekuwa mtumishi wa kuwaongoza na siyo bosi, na pia awe mtu atakayewaongoza kwa uadilifu.

Sifa nyingine za kiongozi huyo ni kuwa mzalendo wa dhati anayejua Watanzania walipotoka, wanapopitia na wanakoelekea; mwaminifu, mjasiri, mtiifu wa sheria na katiba na anayeheshimu mipaka ya cheo chake.

MWANANCHI

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Sepp Blatter ametangaza kuwa atajiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na kashfa ya rushwa iliyolikumba shirikisho hilo.

Akitangaza uamuzi huo, Blatter mwenye miaka 79 alisema baada ya kuitisha mkutano wa dharula wa Fifa: ”Muda mfupi ujao kunatakiwa kuchaguliwe rais mpya.”

Blatter alichaguliwa wiki iliyopita kuliongoza shirikisho hilo, licha ya wajumbe saba wa juu wa Fifa kukamatwa na maafisa usalama wa Marekani siku mbili kabla ya uchaguzi huo.

Blatter alisema: “Uamuzi huu hauungwi mkono na kila mtu.”

Awali Fifa ilikanusha madai kwamba katibu wao mkuu, Jerome Valcke alihusika katika kashfa ya ufisadi ambapo hongo ya mamilioni ya dola ilitolewa.

Fifa inasema hamna afisa wake yeyote wa ngazi ya juu aliyehusika kwa njia yoyote katika kashfa hiyo.

Inasemekana malipo hayo ya rushwa yalitolewa na serikali ya Afrika Kusini kwa maafisa wa soka wa huko Marekani ili waunge mkono wenzao Waafrika waliong’ambo katika nchi za visiwa vya Caribbean.

Waendesha mashtaka wa Marekani wanasema hongo hiyo ilinuiwa kusaidia kununua kura kuiwezesha Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia lililofanyika mwaka 2010.

Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.

Tupia Comments