MWANANCHI
Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bunda, baada ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kutishia kuwa hawatakipigia kura kutokana na kiongozi huyo kutoa ahadi hewa ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Wakazi hao wameapa kuwa labda ahadi hiyo iliyotolewa na Waziri Pinda Machi mwaka jana, itekelezwe kabla ya Uchaguzi Mkuu, kinyume cha hivyo hawataipigia kura CCM ili kuonyesha kuwa hawaridhiki na namna wanavyodanganywa.
Wakazi hao walitoa tishio hilo juzi katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo, Katibu wa CCM mkoa wa Mara Adam Ngalawa na Naibu Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mfaume Kizigo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano huo, walisema, wameazimia kutoipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa kuwa viongozi wa CCM na Serikali yake wanatoa ahadi za uongo na zisizotekelezeka.
Michael Kweka alitaja ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda Machi mwaka jana kwamba tatizo la maji lingekoma Juni, kuwa ni moja ya ahadi hewa za viongozi wa Serikali ya CCM zinazowachefua wananchi.
“Hatutawapigia kura za urais, ubunge wala udiwani wagombea wote watakaoletwa na CCM mwaka huu kwa kuwa wanakuwa wakitudanganya kwa ahadi hewa,”Kweka.
Kweka alisema akiwa ziarani wilayani Bunda Machi mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa ahadi kwamba tatizo la maji lingekwisha ifikapo Juni mwaka huu, lakini hadi sasa hakuna dalili zozote za kumaliza kero hiyo.
Alisema hali hiyo inawafanya wakazi wa mji huo ambao wamekuwa wakidamka nyakati za usiku kutafuta huduma ya maji safi na salama kuichukia Serikali ya CCM, wakiamini kuwa haiwajali. “Mimi kero yangu ni maji. Hiki kimekuwa kilio chetu kwa muda mrefu.
Lakini kinachotuumiza ni ahadi hewa za viongozi wa Serikali ya chama chetu cha Mapinduzi kuhusu mradi unaotekelezwa hapa. Mnaonaje tukiwanyima kura sababu mmezidi ubabaishaji,” alisema mkazi mwingine wa eneo hilo akiwahoji viongozi wa CCM waliokuwapo meza kuu.
Nyerere Lucas aliilalamikia Serikali ya CCM kwa kile alichoeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi zake za kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo kama ilivyoahidi katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kuwafanya wakazi wa maeneo hayo kusafiri kwa tabu kutafuta maji mbali na maeneo yao. Kero nyingine walizolalamikia wakazi wa wilaya hiyo ni mikopo kwa vijana na akinamama.
Walisema mikopo kwa makundi hayo imekuwa ikitolewa kwa watu maaalum hasa vikundi vinavyomilikiwa na watumishi wa serikali, jambo ambalo limeonekana kwamba kuna nia ya dhati ya kuwasahau wananchi.
Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoa wa Mara, Adam Ngalawa katika majibu yake ameshindwa kueleza lini mradi huo wa maji utakamilika badala yake akasema umepangwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka
MWANANCHI
Wanasiasa wanaojiandaa kuingia katika Uchaguzi Mkuu, wametakiwa kumuomba Mungu ili awape nafasi hizo kwa njia sahihi kuliko kutumia ‘sangoma’.
Wito huo ulitolewa jana na Mchungaji Samuel Mshana kwa niaba ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma katika ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Eugen Mwaiposa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga (CCM).
Mwaiposa alifariki dunia juzi akiwa usingizini kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, mwili wake ulisafirishwa jana kwa ndege ya kukodi kupelekwa Dar es Salaam ambako utazikwa keshokutwa nyumbani kwake Kipunguni, Dar es Salaam.
Ilikuwa ni siku ya huzuni jana, wakati wa ibada iliyofanyika kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma, iliyohudhuriwa na umati wa waobelezaji wakiwamo wabunge, wafanyakazi, viongozi wa mkoa na Taifa akiwamo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Katika Bunge la kumi, huyu ni mbunge wa saba kufariki dunia.
Akihutubia kwenye ibada hiyo, Mchungaji Mshana alisema ni wakati wa kuangalia namna watu wanavyopaswa kutafuta madaraka kupitia njia zisizofaa.
Serikali katika ibada hiyo iliwakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Jenister Mhagama, ambaye alisema hadi Mwaiposa kabla ya kukutwa na umauti alionekana mwenye afya njema na aliomba kuchangia katika hotuba ya Wizara ya Afya. Mhagama alisema, Serikali na Chama cha Mapinduzi vimepoteza mtu mahiri ambaye pengo lake halitazibika na kutoa rambirambi ya Sh5 milioni.
MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akieleza kuwa anataka kulifanyia Taifa mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kusimamia Muungano, kukamilisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya, kuweka mfumo wenye motisha kwa wote ili kuchochea uchumi endelevu na wa viwanda, vita dhidi ya rushwa na kukiimarisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kiuchumi.
Sitta alitangaza nia hiyo jana kwenye Ikulu ya Wanyanyembe iliyopo Itetemia, takriban kilomita saba kutoka mjini Tabora.
“Ili kukomesha tatizo hilo (la rushwa), hatuna budi kutunga sheria itakayotenganisha biashara na uongozi,” Sitta alisema akiungana na Rais Jakaya Kikwete ambaye pia aliwahi kuahidi kutenganisha siasa na biashara lakini hadi sasa bado hajatunga sheria hiyo.
“Mtu achague moja, biashara au uongozi wa siasa. Ikiwa mfanyabiashara atataka kuingia katika uongozi wa siasa itabidi akabidhi mali na biashara zake kwa mdhamini atakayeziendesha wakati mhusika anatumikia umma,” alisema Spika huyo wa Bunge la Tisa.
Alisema mikataba mibovu ya huduma na mauzo, ununuzi hewa, ununuzi uliojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni kwa rushwa na hasa rushwa katika ajira, imelisababisha Taifa hasara kubwa.
Alisema hatua ya pili ya kupambana na rushwa ni kutunga sheria mpya zilizo kali na ambazo zitakuwa na matokeo ya kumzuia mtu asitamani kusaka rushwa.
“Katika hilo tutahakikisha mali za viongozi zinatajwa kwa uwazi. Mali isiyolingana na kipato na kukosa maelezo ya kutosheleza itaifishwe, kesi za rushwa ziwe na utaratibu wenye uwazi,” alisema mbunge huyo wa Urambo Mashariki.
“Tume inayoshughulikia maadili ya viongozi ipewe nguvu kubwa za uchunguzi na ufuatiliaji wa mali za viongozi bila kuzuiliwa na mamlaka yoyote. Pia Tume ifanye kazi zake kwa kuyaweka mambo wazi kuhusu watuhumiwa, tuhuma zao, majibu yao na hatua zinazofuatia. Vikao vya tume vya kusikiliza mashauri ya maadili viwe vya wazi kwa wananchi.”
Alisema adhabu ya utoaji na wapokeaji rushwa itakuwa kali na iambatane na mali zitakazothibitika kupatikana kwa rushwa, zitataifishwa.
NIPASHE
Mji wa Dodoma na viunga vyake, leo unatarajiwa kuwaka moto baada ya vigogo sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watakapokuwa wanachukua fomu ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vigogo wanaochukua fomu leo ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Mawaziri Wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na Balozi Ali Abeid Karume.
Mbali ya vigogo hao sita, pia yupo kada mwingine wa chama hicho, Amosi Siyatemi, anayelezwa kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Idadi hiyo ya wanaochukua fomu za kuomba kuwania urais itafikisha jumla ya makada 11 wa CCM ambao tayari wamekwisha kuchukua fomu za kuomba ridhaa kwa chama chao kuwania nafasi ya juu ya uongozi nchini.
Wengine waliochukua fomu jana ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na Balozi Amina Salum Ali.
Lowassa alitakiwa kuchukua fomu jana, lakini aliahirisha kutokana na msiba wa Mbunge wa Ukonga, marehemu Eugen Mwaiposa, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia juzi mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, wa kwanza kuchukua fomu atakuwa Siyatemi, akifuatiwa na Sumaye, Dk. Bilal, Balozi Karume, Lowassa na atakayefunga dimba ni Dk. Magufuli.
NIPASHE
Zaidi ya tembo 10,000 katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa wamepotea ama hawajulikani walipo.
Akitangaza matokeo ya sensa ya tembo ya mwaka 2014 mjini hapa jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema wataalam wa hifadhi wameshindwa kubaini waliko au nini kimewatokea tembo hao na kulinganisha kupotea huko sawa na ilivyotokea kwa ndege ya Malasia Machi mwaka huu ambayo haijaonekana hadi leo.
Sensa hiyo ilifanywa na Shirika la Taifa la Utafiti Wanyamapori (TAWIRI), Frankfurt Zoological Society na Vulcan Inc katika eneo la kilomita za mraba 268,692 ambazo ni sawa na asilimia 28.3 ya eneo lote la nchi, kuanzia Mei hadi Novemba 2014.
Maeneo ilikofanyika sensa hiyo ni Serengeti, Tarangire-Manyara, Katavi-Rukwa, Burigi-Biharamulo, Malagarasi-Muyovosi, Soulus-Mikumi na Ruaha-Ruangwa, Mkomazi na Saadani.
“Wizara yangu inajipanga kikamilifu kujua sababu za kupotea kwa tembo hao…je?, waliuawa au waliondoka katika eneo la hifadhi?. Kwa kawaida kama kuna idadi kubwa ya vifo vya wanyama kama hiyo kunakuwa na mabaki ya mizoga au mifupa kitu ambacho hakijaonekana tangu kupotea tembo hao,” alisema.
Idadi ya tembo katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa imepungua kutoka 20,000 mwaka 2013 hadi kufikia 8,272 mwaka 2014.
“Tembo 10,000 katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa hawajulikani walipo na wala mizoga yao haijaonekana, wamepotea kama ile ndege ya Malasia. Hali hii inatufanya kuendesha sensa nyingine majira ya kiangazi kuanzia Agosti hadi Novemba, wataalam wanajiuliza kila siku tembo hao wamepotelea wapi, hizi ni habari zinazosumbua,” alisema.
Aidha, alisema matokeo ya sensa hiyo pia yamebaini kuwapo kwa upungufu mkubwa katika mfumo wa ekolojia ya Ruaha-Rungwa.
Akitangaza matokeo ya ujumla ya sensa hiyo, Nyalandu alisema imeonyesha kupungua kwa tembo kutoka 110,000 mwaka 2009 hadi 43,330 mwaka 2014.
Hata hivyo, waziri huyo alisema idadi ya tembo imeongezeka kutoka 13,000 mwaka 2013 hadi 15,217 mwaka jana, ongezeko ambalo ni zaidi ya tembo 2,000.
MTANZANIA
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, ameibuka na kusema hajawahi kumshambulia kwenye mitandao Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu sakata la Richmond.
Kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe imekuja siku chache baada ya kusambazwa kwa waraka unaodaiwa kuandikwa naye, ukimuhusisha na tuhuma za kumshambulia Lowassa, jambo ambalo amelifananisha kuwa ni sawa na siasa za kitoto.
Alisema kutokana na kusambazwa kwa waraka ambao umeandikwa nyadhifa zake za ubunge na uwaziri, hivi sasa ameshaanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu waliokuwa wakiusambaza.
Waziri Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanahabari, alisema anapata shaka hata na baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao hiyo na kudai kuwa anamshambulia Lowassa.
“Ninashangazwa sana na hii mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari (magazeti), vimekuwa vikiandika vitu vibaya ikiwa ni pamoja na kumshambulia Lowassa wakati hata siku moja sijazungumza nao.
“Kitendo cha baadhi ya watu wa aina hii kuwaandika vibaya wanasiasa katika mitandao ya kijamii kwa kutumia majina ya watu wengine ni ishara ya woga wa kisiasa na kushindwa kujiamini katika misimamo yao.
“…Kinachonikera kupindukia ni kuwa taarifa hizo sijawai kuziandika ila kuna mtu ama kundi maalumu la watu limeziandika na kuweka jina langu na nafasi zangu za uongozi kama mbunge na waziri, huu si uungwana na wala si siasa kwa kuchezea majina ya watu. Kama siasa zimefika huku basi ni za hatari,” alisema.
Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela mkoani Mbeya, alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, watu wanapaswa kuacha woga na kutojiamini.
“Kitendo cha kutumia majina ya watu na kuelezea hisia zao ni kukosa ujasiri na hata yanayosambazwa kwenye mitandao hayaendani na hadhi yangu kiongozi, sina tabia ya woga na uongo,” alisema.
Alisema baada ya kupata taarifa zilizopo mitandaoni alilazimika kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandaoni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kulalalimikia mchezo huo mchafu.
Dk. Mwakyembe alisema vyombo hivyo vimeshaanza uchunguzi mkali ili kuwabaini watu walioandika na kutuma taarifa hizo.
Alisema kutokana na hali hiyo, amedhamiria na kuhakikisha kesi ya kwanza ya matumizi mabaya ya mitandao inaanzia kwake kwa kuwa hana utamaduni wa woga, na watu wanapaswa kuwa wazi endapo wanakuwa na vitu na si kutumia majina ya watu.
Dk. Mwakyembe alisema anashangazwa na watu kutumia jina lake kumchafua kwa kuwa hana tatizo na mtu yeyote na kama chanzo ni suala la Richmond, ilikuwa ni kazi aliyopewa na Bunge.
MTANZANIA
Baadhi ya wagonjwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wamelalamikia hatua ya uongozi wa hospitali hiyo kushindwa kuchukua hatua za dharura za kutoa huduma za CT-Scan, ambayo imeharibika kwa kipindi cha miezi miwili sasa.
Wagonjwa hao walisema wamekuwa wakiteseka kwa kipindi cha miezi miwili sasa bila kupata huduma hiyo.
Mmoja wa wagonjwa hao aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Omari, alisema ni mwezi wa pili sasa amekuwa akienda na kurudi hospitalini hapo bila ya kupata huduma.
“Kila nikifika bado nakutana na bango la ujumbe unaosomeka mashine ni mbovu mafundi wanafanya matengenezo, nimekuwa nikienda na kurudi huku tatizo likizidi kukuwa, mpaka sasa sijui hatima yangu itakuwaje,” Omari.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha, alikiri kuharibika kwa mashine hiyo na kusisitiza kuwa tayari uongozi umeshaagiza kifaa cha mashine hiyo kutoka nchini Afrika Kusini.
“Tunatarajia kifaa hicho kitafika haraka iwezekanavyo ili kuweza kuwapatia huduma ya kipimo cha CT-Scan wagonjwa wetu wanaokuja kwa ajili ya kufanyiwa kipimo hicho,” ligaesha.
MTANZANIA
Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limemvua uanachama mjumbe wake kutoka Mkoa wa Shinyanga, Chifu Lutayosa Yemba.
Chifu Yemba ambaye pia alikuwa ni mpinzani wa Prof. Ibrahim Lipumba katika kuwania uenyekiti wa CUF kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka jana, alivuliwa uanachama kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama pamoja na kutumia vibaya jina la mwenyekiti wa chama hicho.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho cha Baraza Kuu kilichoanza vikao vyake jana jijini Dar es Salaam, kilisema kuwa tuhuma za mjumbe huyo zilifikishwa mbele ya kikao hicho na kufikiwa uamuzi huo.
“Kikao cha Baraza Kuu bado kinaendelea hapa na ajenda kubwa ilikuwa ni tuhuma dhidi ya Chifu Yemba ambaye anadaiwa kutumia jina la Mwenyekiti wa chama kuanzisha Saccos na hata kusababisha chama kudaiwa shilingi milioni 12.
“Lakini pia amekuwa akitumia jina la Mwenyekiti wa chama, Profesa Lipumba katika mradi wake huo binafsi ambao anauendesha na hata kusababisha chama kuingia katika mgogoro hasa katika Mkoa wa Shinyanga,” kilisema chanzo hicho.
Chifu Yemba alipambana na Profesa Lipumba katika uchaguzi wa kuwania nafasi ya uenyekiti ambapo alipata kura 30 huku Lipumba akishinda kwa kura 659 na kufanikiwa kukiongoza tena chama hicho.
Chanzo hicho kilisema baada ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuvuliwa uanachama kwa Mjumbe huyo wa Baraza Kuu, alitolewa nje ya ukumbi kwa ulinzi maalumu hadi nje ya geti na kuondoka.
Yemba kwa muda amekuwa haelewani na hata kushambuliana katika mitandao ya kijamii na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya ambaye hivi karibuni alishindwa kura za maoni za kuwania ubunge wa Jimbo la Kinondoni.
Kutokana na kushindwa huko kwa Kambaya, kuliibua hisia mbalimbali miongoni mwa wana CUF hali iliyosababisha baadhi ya kikundi cha watu kuandamana na kwenda Makao Makuu ya CUF kufikisha malalamiko yao kuhusu mwenendo wa uchaguzi Kinondoni.
Alipotafutwa Naibu Mkurugenzi wa Habari wa Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alithibitisha kuvuliwa uanachama kwa Chifu Yemba na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.