Magazeti

#Storikubwa MAGAZETINI JUNE09…MEMBE aukana undugu na JK, TIBAIJUKA azomewa mbele ya KINANA na LUKUVI ashusha kodi ya ardhi

on

WOLD

MWANANCHI

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka jana alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi wa jimbo lake mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Hali hiyo ilijitokeza jana asubuhi katika Kata ya Nshamba wilayani hapa wakati msafara wa Kinana ulipofika kuzindua mradi wa maji.

Kadhia hiyo ilianza baada ya Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Ally Idd Ame kumkaribisha mbunge huyo ili awasalimie wananchi. Hata hivyo, wananchi hao walianza kuzomea kwa zaidi ya sekunde 40 wakipinga Profesa Tibaijuka kupanda jukwaani, hali iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya, Francis Isack kupanda jukwaani na kutoa kauli ya kiutawala ili kuwanyamazisha wananchi hao.

“Anayetaka kusikiliza abaki na asiyetaka aondoke,” alisema Isack na kuwanyamazisha mamia ya wananchi hao. Baada ya kauli hiyo wananchi walitulia na kuruhusu Profesa Tibaijuka kupanda na kuhutubia kwa muda.

“Kama hamnitaki siyo lazima niwe mbunge wenu, mnaruhusiwa kubadili. Huyo aliyewapa viroba asubuhi hii ili mje mnitie aibu mbele ya katibu mkuu wa chama nawaambia hiyo dhambi itawatafuna,” .

Aliwaambia wananchi hao kuwa anachokifanya ni kuwatumikia na kuwaletea maendeleo, hasa wanawake…

“Mimi sitafuti kazi na wala sina njaa… na kama hela ya kula ninayo. Mimi sigangi njaa na kama mnataka kuwa na kiongozi mganga njaa muwekeni muone atawasaidia vipi,” alisema.

Akihitimisha salamu zake kwa wananchi hao alisema kama wana jambo lao la ziada walifanye lakini wamuache aendelee na jitihada za kuwaletea wanawake maji… “Sina kinyongo na yeyote kwa sababu “I am too sophisticated (mstaarabu). Nipo juu ya mambo madogomadogo yanayowasumbua.”

Mbunge huyo ambaye hivi karibuni aliondolewa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow, alimweleza Kinana kuwa eneo hilo limekumbwa na upinzani kutoka kwa mtu anayehitaji kulichukua ambaye ni kutoka ndani ya CCM.

MWANANCHI

Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed  amesema wimbi la ndoa kuvunjika visiwani hapa limekuwa likisababisha familia nyingi kuishi katika mazingira magumu.

Waziri Mohammed alisema hayo jana alipofunga mjadala wa makadirio na matumizi ya bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2015/2016 katika kikao cha bajeti kilichofanyika Chukwani, Zanzibar.

Alisema ndoa zinapovunjika watoto wanakosa haki zao za msingi ikiwamo elimu, huku wanawake wakiishi katika mazingira magumu.

Waziri Mohammed alitaja sababu za ndoa hizo kuvunjika kuwa ni migororo ya wanandoa, udhalilishaji, kukosa uaminifu na watoto kutopewa matunzo.

Hata hivyo, alisema wizara inalifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na viongozi wa dini na jamii ili kupunguza matatizo hayo.

Alisema kwamba kesi nyingi za udhalilishaji wanawake na watoto zinashindwa kupata mwelekeo mzuri katika Vyombo vya sheria kutokana na tatizo la kupatikana kwa ushahidi wa kutosha pamoja na kesi zenyewe kuharishwa mara kwa mara na kuwakatisha tamaa wahusika.

Awali, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Makame Mshimba Mbarouk, Hamza Hassan Juma, Viwe Khamis Abdalla na Wanu Hafidh Ameir walitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kusimamia kesi za unyanyasaji wanawake na watoto.

Hata hivyo, Waziri Mohammed alisema suala hilo linahitaji ushirikiano na mamlaka mbalimbali zinazosimamia sheria.

Pia alisema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano wakati wa upelelezi wa kesi husika ikiwamo kutoa ushahidi mahakamani.

MWANANCHI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inatimiza mipango yake kuelekea katika Uchaguzi Mkuu kutokana na ugumu unaoweza kutokea katika kukamilisha uandikishaji wapigakura katika jiji la Dar es Salaam na ugawaji wa mipaka ya majimbo nchini.

Ratiba ya uandikishaji ya NEC imelipatia jiji la Dar es Salaam siku 13 za kuandikishaji wapigakura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).

Siku hizo ni pungufu kwa wastani wa siku 16 zilizotumika kwenye mikoa mingine nchini ambayo mingi ina nusu ya idadi ya watu wenye umri wa kupiga kura ikilinganishwa na jiji la Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi Mosena Nyambabe aliliambia gazeti hili kuwa ili NEC iendane na kasi ya muda uliopo, inatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inakamilisha uandikishaji wapigakura na ugawaji wa mipaka ya majimbo.

“Uzuri wa Dar es Salaam ni makao makuu ya kila kitu, tutaangalia mwenendo wa uandikishaji kujua unafanyika kikamilifu au la na utatupa picha hali ilikuwaje katika mikoa mingine. Bado wana kazi kubwa kwa sababu hawajakamilisha kuchora ramani ya mikoa na majimbo…lazima wafanye kazi ya kutisha,”  Nyambabe.

Alisema kazi ya mwaka mmoja na nusu haiwezi kufanyika ndani ya wiki mbili ndiyo maana wakati mwingine huwa wanaona mipango ya NEC kama viini macho. Hata hivyo akasema angalau sasa NEC wamejikita katika Uchaguzi Mkuu kuliko Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.

Takwimu za Shirika la Takwimu la Taifa (NBS) za makadirio ya watu wenye sifa ya kupiga kura zinaonyesha kuwa Dar es Salaam ina zaidi ya watu 2.93 milioni, idadi ambayo ni sawa na jumla ya wapigakura katika mikoa sita ya Katavi, Lindi, Shinyanga, Njombe, Iringa na Rukwa ambao wanakadiriwa kuwa 2.94 milioni.

NBS inakadiria Morogoro kuwa na wapigakura zaidi ya 1.28 milioni wakati Tanga ina watu zaidi ya 1.12 milioni.

MWANANCHI

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ameanza ziara ya siku nane barani Ulaya ambako atashiriki mijadala kuhusu hali ya demokrasia na kukutana na jopo la wataalamu wa masuala ya uchumi kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika kupata mifumo sahihi na kujenga taasisi za kusaidia uwajibikaji na kusukuma maendeleo ya watu.

Katika ziara hiyo ya tatu baada ya mbili alizofanya Marekani, Dk Slaa anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu hali ya demokrasia, utawala bora na hali ya haki za binadamu nchini hasa kwa kipindi hiki ambacho Watanzania wanaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho, Deogratias Munishi ilisema: “Katika ziara hiyo, viongozi hao wa Ulaya watapata fursa ya kujadiliana na Dk Slaa hali ya siasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki.”

Dk Slaa ambaye aliondoka Jumamosi iliyopita, ameongozana na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa chama hicho, John Mrema na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, ameanza ziara akiwa ametoka katika mikoa ya Kagera, Mbeya, Rukwa na Katavi akikagua uandikishaji wapigakura kwenye kwa mfumo wa BVR na kuhamasisha wananchi wenye sifa kujiandikisha.

Kiongozi huyo ambaye anatajwa kuwania nafasi ya urais ndani ya Ukawa, anafanya ziara hiyo ukiwa umepita mwezi mmoja na nusu tangu alipofanya ziara ya pili nchini Marekani.

Aprili 13 mwaka huu, Dk Slaa alianza ziara ya siku tisa Marekani ambako alishiriki mijadala inayohusu uwekezaji, elimu na uongozi ikiwa na lengo la kuitangaza Tanzania.

Katika ziara hiyo alifanya mihadhara kwenye vyuo vikuu vya Purdue, Indianapolis na Marion pamoja na vikao vya mashauriano na baadhi ya wahadhiri wa vyuo hivyo kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya kisiasa na maendeleo, kijamii na ushiriki wa Chadema katika siasa za kimataifa.

Pia, alikutana na viongozi wa taasisi pamoja na kampuni kubwa za uwekezaji kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika usimamiaji wa masuala ya uchumi na uwekezaji Afrika na kipekee kwa Tanzania.

Septemba 21, 2013, Dk Slaa alifanya ziara ya wiki tatu nchini humo na alitembelea majimbo mawili ambako alizungumza na Watanzania waishio Marekani na kukutana na viongozi pamoja na kutembelea vyuo vikuu kadhaa katika majimbo ya North Carolina na Alabama.

Dk Slaa alihutubia katika Chuo Kikuu cha Stamford ambako aliutangaza utalii na fursa za uwekezaji nchini, akisema Tanzania ni nchi tajiri isiyohitaji misaada kutoka popote kama haijapatwa na janga.

“Viongozi wengi wa Afrika wanaaminika kwenda Ulaya na Marekani kuomba misaada. Hii imewajengea taswira kuwa Waafrika wengi ni maskini na wavivu. Lakini ukweli ni kwamba Afrika ipo katika kipindi cha mpito kujitegemea kwa kila kitu. Sijaja hapa kuomba kwa sababu nchi yangu ni tajiri sana,”  Dk Slaa

MWANANCHI

Serikali imefuta umiliki wa baadhi ya mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa na wawekezaji na kuyakabidhi kwa wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara yake katika kipindi cha 2015/2016.

Lukuvi alisema migogoro mingi kati ya wananchi na wamiliki wa mashamba, wananchi na hifadhi za Taifa imepungua baada ya mipaka kurekebishwa.

Rais amefuta umiliki wa shamba la Ufyomi Galapo Estate na kazi inayoendelea kwa sasa ni kuhakiki, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili waweze kuitumia,”Lukuvi.

Aliyataja mashamba mengine kuwa ni Utumaini la Halmashauri ya Wilaya ya Mafia lenye ukubwa wa ekari 4,040 pamoja na shamba la Malonje katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.

Waziri Lukuvi alisema bado kuna changamoto nyingi za mashamba ambayo wananchi wanataka umiliki wake ufutwe.

Kuhusu umilikaji wa ardhi, alikiri bado kuna tatizo katika maeneo mengi nchini ambayo licha ya viwanja kupimwa, bado halmashauri zinashindwa kuandaa michoro na hati za kuwapa wananchi wanaohitaji viwanja hivyo.

Akizungumzia Mji wa Kigamboni katika Jiji la Dar es Salaam, alisema wizara baada ya kuchunguza imeona kuna haja ya kupunguza eneo hilo baada ya marekebisho ya Tangazo la Serikali.

“Eneo la mpango limepunguzwa kwa kuondoa kata tatu za Mpiji, Pembamnazi na Kisarawe ambalo lina ukubwa wa hekta 44,440 ambazo hazikuwapo katika mpango wa awali, hivyo kubaki na kata sita zenye ukubwa wa hekta 6,494,” Lukuvi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli aliitaka Serikali kusimamia kauli yake kwamba haiwezekani kupima ardhi kama haijawalipa fidia wamiliki wa maeneo hayo.

MTANZANIA

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, amehusishwa na tuhuma za kutaka kumiliki ardhi kwa njia za kifisadi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Wilaya ya Rombo mkoani humo.

Kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuzuia mchakato wowote haramu utakaofanywa na Gama kuhusu ardhi.

RC Gama, alitajwa bungeni na Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee (Chadema) wakati akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2015/16 mjini Dodoma jana.

Alisema Gama anashirikiana na kampuni binafsi ya Jun Yu Investment International, anataka kumiliki ardhi iliyokwishalipiwa fidia ya Sh milioni 168 na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe jijni Dar es Salaam, katika hotuba yake, aliambatanisha vielelezo vinavyomwonyesha Gama kuhusika katika kampuni hiyo.

Aliwataja wahusika wengine kuwa ni Wang Zhigang raia wa China anayemiliki hisa 48,000, Feng Hu raia China mwenye hisa 49 na Muyanga Leonidas Gama ambaye ni mtoto wa Gama anayemiliki hisa 3,000.

“Habari tulizonazo, mkuu wa mkoa anamiliki hisa 20,000 ambapo hisa 10,000 zimefichwa kwa mwanahisa wa kwanza na 10,000 nyingine kwa mwanahisa wa pili kupitia mkataba wa pili uliofichwa, ambao pia tumeuambatanisha katika hotuba hii.

“Katika hali ya kushangaza, Halmashauri ya Rombo ambayo iliwekeza fedha zake Sh milioni 168 haitambuliwi na wala haina hisa hata moja katika kampuni hiyo,” alisema Mdee.

Alisema kambi ya upinzani ina taarifa za kiintelijensia ambazo zinaonyesha wawekezaji hao wa kichina walilipa Sh milioni 500 kama fidia kwa wananchi katika ardhi hiyo ambayo Halmashauri ya Rombo ilishalipa Sh milioni 168, lakini fedha hizo hazijulikani zilipo.

Mdee, pia alimtaja Gama kutaka kufanya ufisadi katika eneo lililopo Kilalacha ambalo linagusa Jimbo la Vunjo na Rombo lenye ukubwa wa hekta 2,700.

Akizungumzia suala hilo, Mdee alisema eneo hilo lilikuwa mali ya ushirika uliokuwa ukifahamika kwa jina la Lokolova, lakini katika siku za karibuni kigogo huyo wa mkoa amekuwa akilinyemelemea kwa kisingizio cha uwekezaji.

Alisema Gama yupo nyuma ya mgogoro wa ardhi unaokihusisha kiwanja cha Mawenzi chenye hati namba C.T 056035 kilichokuwa chini ya miliki ya The Registered Trustees of Mawenzi Sport Club.

“Kiwanja hiki kilikuwa na hatimiliki ya miaka 33 iliyokwisha mwaka 1974. Mwaka 1994 kupitia kwa aliyekuwa waziri wa ardhi wakati huo, Edward Lowassa, alitoa amri ya kutwaa maeneo mbalimbali likiwamo hilo.

“Hali ilikuwa salama kwa wakuu wote wa mikoa waliopita, lakini hali ilibadilika alipoletwa Gama ambaye amekuwa akitumia ofisi yake kushinikiza kiwanja husika kikabidhiwe kwa matapeli ambao wametengeneza nyaraka feki na kuziwasilisha kwa Wakala wa Udhamini na Ufilisi (RITA) na kujitambulisha kama wadhamini wapya baada ya kukabidhiwa na wadhamini wa awali.

“Wakati matapeli hawa wanaotambulika kwa majina ya Amratlal N. Pattn na Hittesh H. Solan wakionyesha kikao cha makabidhiano kilifanyika Januari 5, 2008 mbele ya wadhamini wa awali, Devchad Nathu Shah na Mohamedal Sharriff, taarifa za uhakika ni kwamba Shah alishafariki dunia tangu mwaka 1979 wakati Sharriff alifariki mwaka 1998,” alisema Mdee.

Awali akitoa hotuba ya makadirio ya wizara yake kwa mwaka 2015/2016, Waziri Lukuvi alionya makundi yanayochukua ardhi ya wananchi kwa ajili ya matumizi mbalimbali kutokulipa fidia kwa mujibu wa sheria.

Alisema watumishi wa sekta ya ardhi, watakaobainika kusababisha kero kwa wananchi, hususan katika halmashauri nchini, watachukuliwa hatua ikiwamo kufukuzwa kazi.

NIPASHE

Mbunge wa Muleba Kusini mkoani Kagera, Profesa Anna Tibaijuka, amesema kushindwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika baadhi ya mitaa na vijiji kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba, mwaka jana, hakukutokana na sakata la fedha za Escrow.

Profesa Tibaijuka alisema sababu ya kuanguka kwa wagombea ni mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho na mivurugano waliyonayo ya ndani Chama.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Muleba na kufafanua kuwa kuna baadhi ya maeneo chama chake kimeshindwa katika wilaya hiyo lakini si kwa sababu ya Escrow kwani amejiridhisha baada ya kufanya utafiti wa kisiasa.

Alisema kuwa yeye ni Mbunge wa Buleba Kusini lakini wagombea walioanguka kwenye uchaguzi huo ni wa Muleba Kaskazini ambako hawahusiki na sakata la Tegeta Escrow.

“Nimefanya utafiti mdogo na takwimu zinanionyesha kuwa chama chetu hakijaangushwa kwenye uchaguzi kutokana na sakata la Escrow bali kutokana na maneno ya makada wake tunapaswa tubadilike mapema kwani tusipofanya hivyo tutapoteza viti vya madiwani na wabunge,” alionya Profesa Tibaijuka ambaye Rais Jakaya Kikwete, alimuondoa katika nafasi ya Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kuhusishwa na kashfa ya fedha za Tegeta Escrow.

NIPASHE

Katika halia isiyo ya kawaida, Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho ya Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) visiwani Zanzibar, Sheikh Ahmed Farid na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kula njama na kujihusisha ya ugaidi nchini waligoma kushuka kwenye basi la magereza ili kuingia mahakamani jana kutokana na hatma ya upelelezi wa kesi yao kutojulikana.

Washtakiwa hao walifikishwa kwenye viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam saa 2:50 asubuhi kwa ajili kusikiliza kesi yao iliyopangwa kutajwa jana.

Kabla ya mgomo huo, washtakiwa hao wanaotoka visiwani Zanzibar, waliiomba mahakama kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuwatembelea mahabusu kwa ajili ya kusikiliza kero zao kuhusiana na kushitakiwa kwao katika mahakama za Tanzania Bara badala ya mahakama za kwao, Zanzibar.

Viunga vya mahakama hiyo vilifurika askari kanzu na wenye sare za Jeshi la Polisi pamoja na wa Jeshi la Magereza kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.

Hata hivyo, baada ya kufikishwa mahakamani hapo washtakiwa wote 23 waligoma kushuka kwenda kusikiliza kesi yao kwenye ukumbi wa mahakama hiyo.

Saa 4:56 asubuhi, mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Renatus Rutatinisibwa, huku upande wa Jamhuri ukiongozwa na mawakili wa serikali, Peter Njike na George Barasa, wakisaidiana na wakili wa serikali mwandamizi, Tumaini Kweka.

Wakili Njike alidai kuwa washtakiwa wamegoma kushuka kwenye basi la Jeshi la Magereza tangu wafikishwe mahakamani hapo kutoka mahabusu.

Wakili wa utetezi, Abdallah Juma, alidai kuwa upande wao hauna taarifa kuhusiana na  washtakiwa kugoma kuingia mahakamani na kwamba, upande wa Jamhuri ndiyo una wajibu wa kujua chochote kuhusu washtakiwa waliopo mahabusu.

Wakili Kweka, alidai kuwa askari magereza wamefanya juhudi za kuwataka washuke kwenye basi ili kuingia mahakamani lakini imeshindikana.

“Mheshimiwa, Mei 25 mwaka huu, mahakama yako ilitoa amri kwamba kesi hii itatajwa leo… Jamhuri tunaomba washtakiwa wahesabike kwamba hawajafika mahakamani. Pamoja na kwamba wapo katika viunga vya mahakama, tunaomba mahakama itoe amri wapangiwe tarehe nyingine na wafike mahakamani,” alidai Wakili Kweka wa upande wa Jamhuri.

Hakimu Rutatinisibwa alisema mahakama haiwezi kuwafuata washtakiwa nje ya ukumbi unaoendesha shughuli zake na kwamba, (mahakama) inaendesha kazi zake kwa mujibu wa sheria, hivyo inaahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu itakapotajwa tena.

Mbali na Sheikh Farid, watuhumiwa wengine ni Noorid Swalehe, Ally Hamis Ally, Jamal,   Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan,  Hussein Mohamed,  Juma Sadala,  Said Kassim,  Hamis  Amour,  Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othuman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe pamoja na wenzao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kuingiza watu nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi,, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya  kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.

Ilidaiwa kuwa  katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini,  Sheikh Farid na Sheikh Mselem Mselem waliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.

Shekh Farid anadaiwa kuwa katika kipindi hicho, akiwa anajua kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.

Baaada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

NIPASHE

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, amekana kuwa na undugu wa damu na Rais Jakaya Kikwete.

Membe ambaye ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na kisha jana kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea kiti hicho, alisema ingawa amekuwa akifananishwa na Rais Kikwete mara kadhaa; hakuna ushahidi wowote wa kibailojia unaothibitisha kwamba wana uhusiano wa kindugu.

Membe alisema baadhi ya watu wamekuwa wakimfananisha na Rais Kikwete lakini hawana undugu wowote baina yao.

“Kungekuwa na aibu gani au hasara gani kuficha kwamba mimi ni ndugu wa damu wa Rais Jakaya Kikwete. Mimi siyo ndugu wa mheshimiwa Rais, lakini  binadamu tunafanana…rangi yangu, sura yangu na ufupi wangu nimeuchukua kwa mama yangu,” alisema Membe na kuongeza:

”Aliyekuwa Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika (sasa marehemu) wakati fulani pia aliwahi kunifananisha na Rais Kikwete. Naomba nitamke wazi kwamba sina undugu wa damu na mheshimiwa Rais.” 

Alisema hali hiyo pia iliwahi kumkuta baada ya Wamarekani weusi (Afro Americans) kumkaribisha Marekani wengi walimuomba kupiga naye picha wakidhani ni Rais Kikwete lakini baadaye aliwaeleza ukweli kwamba yeye hakuwa Rais Kikwete.

Luhaga Mpina ambaye naye ametangaza nia ya kuwania nafasi ya Urais kupitia chama hicho, alisema akipata ridhaa ya chama chake na baadaye watanzania wakimwamini na kumchagua atahakikisha anasimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali ili yapande mara mbili au tatu zaidi ya sasa pamoja na kusimamia rasilimali za umma ziwanufaishe wanyonge badala ya  wachache.

“Mimi si mdogo wala mtu wa kudharauliwa katika wagombea waliotangaza nia ya kugombea urais. Mkitaka kujua mimi naweza fuatilieni, mimi ndiye mbunge wa kwanza Afrika kusimama hadharani na kuzungumzia utoroshaji wa mabilioni ya fedha kwa nchi za Afrika kwenda ughaibuni.

Ndiye niliyesababisha Afrika ikaunda kamati iliyoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini, Thabo Mbeki kushughilikia suala hilo kwa nchi za Afrika,” alisema Mpina.

Hadi kufikia jana mchana makada wa CCM waliotangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho na kisha kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania kiti hicho walifikia 20

NIPASHE

Mamia ya wananchi katika wilaya za Chato na Geita wamejitokeza kumdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa ajili ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM).

Lowassa aliwasili jana saa sita mchana kwa ndege akitokea Zanzibar na kupokelewa na mamia ya watu na kuelekea wilaya ya Chato, kwenye jimbo la msaka urais mwingine wa CCM, John Pombe Magufuli.

Akiwa Chato, Lowassa alidhaminiwa na wanachama wa CCM 430 wakiwamo wa makundi ya wafugaji, watu wa daladala, waendesha bodaboda. Wanachama wengine wa chama hicho zaidi ya 3,000 wakijitokeza wilayani Geita kwa nia ya kumdhamini.

Lowassa aliwashukuru wanachama hao kwa kumdhamini na pia kwa kuonyesha moyo wa upendo kwake katika hatua hiyo.

Kila anayewania kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais, anatakiwa awe na wadhamini 450 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

“Nimekuja kuleta fomu za kunidhamini na ninashukuru mmenidhamini, mwezi wa kumi mnaenda kuchagua rais na mwenyekiti wa CCM… ndiyo sababu nimekuja kuomba ridhaa yenu,”alisema Lowassa.

Alisema hajafika kuomba kura isipokuwa anawapa angalizo kuhakikisha wanapomchagua mwenyekiti wanaangalia historia yake na amefanya nini.

Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa jimbo la Busega, Rafael Chegeni, alisema mtu pekee ambaye anaweza kuwavusha wananchi walipo ni Lowassa.

NIPASHE

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya chama hicho, Philip Mangula, ametaja sifa 13 muhimu anazotakiwa kuwa nazo mgombea urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Mangula alitaja sifa hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, huku tayari kukiwa na makada 20 waliojitokeza kutangaza nia na wengine tayari wamechukua fomu za kuwania kuwa wagombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

“Mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwa ngazi ya urais umeanza. Kwa ngazi ya ubunge, uwakilishi na udiwani bado mchakato wake haujaanza.

Lakini nazitaja sifa za msingi zitakazozingatiwa kwa mgombea urais, hizi ziko kwenye kifungu cha 5, kifungu kidogo cha (1) hadi cha 13…Na hizi ndizo zitakazotumika kumpata mgombea katika mchakato mzima wa uteuzi ndani ya CCM,” alisema Mangula.

Mangula alizitaja sifa hizo kuwa ni, mosi; Awe na uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa kwa kuzingatia uzoefu wake katika uongozi wa shughuli za serikali, umma na taasisi.

Pili; Awe mwadilifu, mwenye hekima na busara na Tatu; Awe na angalau elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo.

Alitaja sifa ya nne kuwa ni; Awe ni mtu mwenye upeo mkubwa wa kuweza kudumisha muungano, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa uliopo.

Tano; Awe mwepesi wa kuona mbali na asiyeyumbishwa, mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya busara kuhusu masuala nyeti ya kitaifa kwa wakati unaofaa.

Ya sita awe na upeo mkubwa na uwezo usiotiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifa na anayeweza kuwa kiongozi imara atakayetuunganisha na mataifa mengine.

Aliitaja sifa ya saba kuwa ni; Asiwe mtu mwenye hulka ya kidikteta au fashisti, bali awe mtu anayeheshimu katiba, sheria, utawala bora na kanuni zilizopo. 8; Awe ni mtu anayeweza kutetea wanyonge na haki za binadamu na sifa ya tisa; Awe mzingatiaji makini na asiye mtu anayejitafutia umaarufu binafsi.

10; Awe mtu wa mstari wa mbele kuzitekeleza sera na ilani ya CCM na awe ni  mpenda haki na jasiri wa kutetea maslahi ya umma, kupambana na dhuluma na uonevu.

Sifa ya 11, Mangula alisema mgombea wa CCM anapaswa kuwa ni mtu asiyetumia nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali na sifa ya 12 ni lazima awe ni mtu anayekubalika na wananchi na ya 13 ni lazima awe ni mtu makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji.

Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.

 

Tupia Comments